Nahodha wa timu ya Watford, Troy Deeney, amesema hatarejea katika kambi yao uwanjani Vicarage Road kwa mazoezi yanayofanywa sasa na wanasoka wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa minajili ya kampeni zilizosalia msimu huu wa 2019-20. Nyota huyo mzawa wa Uingereza ameshikilia kwamba anahofia uwezekano mkubwa wa kuambukiza familia yake virusi vya corona iwapo atakuwa sehemu ya watakaorudi kambini mwa mazoezi. Amesema kuna hofu miongoni mwa wachezaji, na haoni ni kwa sababu gani kuna haraka ya kuanza tena kwa ligi hiyo, kauli ambayo imeungwa mkono na Mwenyekiti wa kikosi cha Watford, Scott Duxbury. Kwa mujibu wa magazeti mengi ya Uingereza, Deeney ana mtoto aliye na matatizo ya kupumua na huenda akawa katika "hatari zaidi" ya kuambukizwa ugonjwa wa corona ambao umewalemea zaidi wachezaji wenye asili ya Kiafrika na Asia nchini Uingereza. Deeney, Sergio Aguero wa Manchester City na Danny Rose wa Tottenham Hotspur ni miongoni mwa wachezaji ambao wamejitokeza kulalamikia hatua ya kurejelewa kwa kipute cha EPL wakati ambapo janga la corona bado halijadhibitiwa vilivyo duniani.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |