Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amedokeza kuwa nchi hiyo huenda ikafunguliwa hivi karibuni na kuondolewa vikwazo vilivyowekwa ili kudhibiti ueneaji wa maambukizi ya virusi vya Corona.
Akizungumza jumamosi katika hotuba yake ya 7 kwa taifa tangu kutangazwa kwa kisa cha kwanza cha Corona nchini humo,Rais Kenyatta alisema ni muhimu kwa wananchi wa Kenya kurejelea shughuli zao za kiuchumi na kuongeza kuwa taifa haliwezi kuendelea kufungwa kwa muda mrefu.
Rais Kenyatta alisema maamuzi ya kufungua nchi na kuondoa vikwazo kama vile vya kafyu,zuio la kutoingia na kutotoka katika baadhi ya miji na mitaa,kufungwa kwa shule,vyuo,nyumba za ibada pamoja na vikwazo vingine viliyowekwa ili kudhibiti ueneaji wa maambukizi ya Corona utategemea na jinsi watu wanavyoendelea kuchukua tahadhari za kujikinga.
Alisema kila mmoja ana jukumu la kujilinda na kumlinda mwenzake dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.
"Kile kitu ambacho kitatusaidia kwa kikamilifu kuhakikisha ya kwamba tumeweza tena kufungua uchumi wetu na wananchi waweze kuendelea na maisha yao ya kawaida sio kwa sababu ya yale serikali itatenda,itakuwa kwa sababu ya yale kila mmoja wetu kwa kibinafsi atafanya.Wewe uko na jukumu la kuhakikisha umemchunga mwenzako.Usipotii masharti ambayo tumepatiwa sio wewe pekee utakayeumia,unaumiza pia mwenzako kwa kazi ambayo unafanya.Ukienda nyumbani unaumiza mama na mtoto"
Rais aliwahimiza wakenya kuendelea kutii na kufuata kanuni na masharti yaliyotolewa na Wizara ya Afya na Shirika la Afya Duniani,WHO.
"Wakati umefika,na nimewaambia mawaziri na haswa maafisa wetu wa afya waanze kuwaeleza wakenya ya kwamba hatuwezi kuendelea na lockdown,hatuwezi kuendelea maisha na kafyu.Na tukifungua,huu ugonjwa ukianza kuenea,wakenya lazima mjue ya kwamba utaenea kwa sababu sisi wenyewe hatujatimiza yale masharti tuliyopatiwa,lakini tukiyatimiza tutapona.Mimi sina shaka na hilo"
Aidha siku hiyo Rais Kenyatta alitangaza mpango wa hatua nane za uchumi wa Ksh53.7 bn.
Rais Kenyatta alisema serikali imetenga fedha hizo ili kusaidia kufufua uchumi wa nchi kutokana na athari za ugonjwa Corona.
Biashara katika sekta ya utalii zitaweza kupata mkopo kupitia mfuko huo.
Shilingi 5bn zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu.Miundmbinu ya barabara imeharibika kutokana na mvua zinazoendelea kunya kote nchini.
Wizara ya Elimu imetengewa Ksh6.5bn ili iajiri walimu 10,000 na ,1,000 wa teknolojia ya habari na mawasiliano ili kusaidia katika mafunzo ya kidijitali.
Sekta nyingine zilizonufaika na mpango huo ni afya,kilimo,mazingira na maji.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |