• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Umoja wa Afrika walaani mauaji ya Mmarekani mweusi Floyd huku machafuko yakiendelea miji mingi nchini Marekani

    (GMT+08:00) 2020-05-31 19:00:40

    Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat amelaani vikali mauaji ya George Floyd nchini Marekani akiwa mikononi mwa polisi, na kuwapa mkono wa pole familia na wapendwa wake.

    Bw. Mahamat amesisitiza kuwa Umoja wa Afrika unapinga kuendelea kwa vitendo vya kibaguzi dhidi ya raia weusi nchini Marekani na kuzitaka mamlaka kuzidisha juhudi ili kuhakikisha zinaondolewa aina zote za vitendo vya kibaguzi vinavyotokana na rangi au kabila.

    Wakati huohuo nchini Marekani waandamanaji wameingia barabarani siku ya Jumamosi katika miji takriban 30, wakipinga mauaji ya Floyd ambaye hakuwa na silaha yoyote huko Minneapolis, Minnesota. Miji karibu 25 katika majimbo 16 imeweka kafyu huku majimbo zaidi ya manane pamoja na Washington D.C yakiita jeshi la ulinzi wa taifa kusaidia kukabiliana na waandamanaji na vurugu. Na gavana wa jimbo la California Gavin Newsom jana alitangaza hali ya dharura katika kaunti ya Los Angeles ikiwa ni siku ya nne mfululizo ya maandamano juu ya mauaji ya Floyd.

    Hadi sasa, watu zaidi ya 1,400 wamekamatwa katika maandamano hayo kwenye miji 17 tangu siku ya Alhamis.

    Mjini Washington waandamanaji walikusanyika nje ya Ikulu ya Marekani kwa siku ya pili mfululizo, wakisema "mikono juu, usifyatue risasi" na "siwezi kupumua". Magari kadhaa na mapipa ya taka yalichomwa moto karibu na Ikulu, huku polisi wakitumia gesi za kutoa machozi ili kuwatawanya waandamaji.

    Jumamosi mchana rais wa Marekani Donald Trump aliandika kwenye twitter kwamba "kuvuka mstari wa serikali ili kuchochea vurugu ni uhalifu dhidi ya serikali!"

    Minneapolis, mji uliofanyika mauaji, maandamano yameendelea kwa siku ya tano huku waandamanaji wakiwarushia vitu polisi na kupinga tena amri ya kutotoka nje ya mji mzima iliyowekwa kuanzia Ijumaa. Kwenye taarifa yake polisi ya Seattle imesema, baada ya kufanyika maandamano ya Amani kwa saa kadhaa, maandamano hayo yakageuka vurugu na kuanza kuwarushia chupa maafisa wa polisi.

    Floyd mwenye umri wa miaka 46, amefariki Jumatatu baada ya Derek Chauvin, polisi mzungu kumkandamiza kwa goti shingoni mwake licha ya kurejea tena na tena kuwa hawezi kupumua. Chauvin alikamatwa na kushtakiwa kwa mauaji na ukatili siku ya Ijumaa.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako