Kikosi cha Yanga kimeibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Trans Camp inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania katika mchezo wa kirafiki uliopigwa kwenye uwanja wa chuo cha Sheria jana jioni. Yanga ndio walikuwa wa kwanza kupata goli dakika 52 kupitia kwa mshambuliaji wao Bernard Morrison ambaye aliwatoka mabeki wa Transit Camp lakini alifanyiwa madhambi na kuwa penalti ambayo aliipiga na kuingia wavuni. Transit Camp nao hawakuonyesha unyonge kwani walitumia dakika tano tu kurudisha goli walilofunga katika dakika 57 kupitia kwa Prosper Pius aliyepiga shuti kali lililoenda wavuni. Yanga walifanya mabadiliko dakika 67 huku mabadiliko hayo yakionyesha kuwa na tija baada ya dakika 76 kupata goli la pili kupitia kwa Feisal Salum aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa faulo uliopigwa na Juma Abdul. Yanga walionekana kumiliki mpira zaidi huku wachezaji wa Trans Camp wakionekana kuishiwa pumzi katika dakika za lala salama. Dakika ya 89 Yanga walipata goli la tatu kupitia kwa Mrisho Ngassa ambaye alifanya kazi ya ziada kuiwahi pasi ya Yikpe ambaye walipasiana wenyewe kwa wenyewe na kupiga shuti lililojaa wavuni.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |