Takwimu zilizotolewa na Idara Kuu ya Takwimu ya China zinaonesha kuwa, katika mwezi uliopita, viashiria vikuu vya uchumi wa China vimeboreka kwa mfululizo, na uchumi wa China umeendelea kufufuka.
Matumizi ya ndani yameendelea kuongezeka. Baada ya kufanikiwa kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona, mauzo ya bidhaa sokoni nchini China yameongezeka kwa miezi mitatu mfululizo. Hali hii inaonesha kuwa matumizi ya watu bilioni 1.4 bado yataendelea kuwa injini kuu ya ukuaji wa uchumi wa China. Mtafiti mwandamizi wa Benki ya Ujerumani katika eneo la Asia na Pasifiki Michael Spencer anaona kuwa, ongezeko la matumizi ya ndani litasaidia uchumi wa China kukua kwa asilimia 5 hadi 6 katika robo ya pili ikilinganishwa na robo ya kwanza ya mwaka huu.
Licha ya hayo, sekta ya teknolojia ya juu imekuwa injini mpya ya maendeleo ya uchumi wa China. Aina nyingi mpya za uchumi wa kidijitali zimeonesha uhai mkubwa na kukua kwa kasi. Hali hii imethibitisha ufanisi wa juhudi za China kuendeleza teknolojia mpya na za juu katika miaka mingi iliyopita. Sekta hiyo itaendelea kuwa injini kubwa ya ukuaji wa uchumi wa China.
Hivi sasa China imeanzisha mpango mkubwa wa "Ujenzi wa Miundombinu Mipya". Serikali ya China imesisitiza tena kuharakisha mchakato wa ujenzi wa mtandao wa 5G na vituo vya data, na kuunga mkono sera kwa marekebisho ya mnyororo wa ugavi. Hatua hizo zitahimiza kuinua kiwango cha mnyororo wa ugavi duniani, na kuongeza mvuto wa soko la China.
Kampuni ya KPMG hivi karibuni imetoa ripoti, ikikadiria kuwa uchumi wa China utaendelea kudumisha mwelekeo wa kufufuka katika robo ya pili ya mwaka huu. Watafiti wa Kampuni ya Uwekezaji ya Marekani BlackRock pia wanaona kuwa, uchumi wa China umefufuka kwa kasi zaidi kuliko ulivyotarajiwa na baadhi ya watu, na utarudi kwenye njia ya kukua kama awali kabla ya kutokea kwa mlipuko wa virusi vya Corona.
Hivi sasa, kutokana na kuhamasishwa kwa shughuli za kurejesha uzalishaji wa kawaida, kuonesha kwa ufanisi wa sera ya serikali, na ongezeko la injini mpya, maendeleo ya uchumi wa China yana mwelekeo mzuri katika siku zijazo. Wakati huohuo, uchumi wa China pia unakabiliwa na matatizo ya muundo, mfumo na yale yanayorudia kila baada ya muda. Mbali na hayo, uchumi wa China pia unakabiliwa na athari ya virusi vya Corona, udhaifu wa mnyororo wa ugavi duniani, na vitendo vya kujilinda kibiashara. Hivyo China inapaswa kufanya juhudi kubwa zaidi, ili kuendeleza uchumi wake, na kusaidia uchumi wa dunia kufufuka.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |