Mabalozi wa China katika nchi kadhaa za Afrika hivi karibuni wamesema, tangu kutokea kwa mlipuko wa virusi vya Corona, China na Afrika zimeshirikiana kukabiliana na virusi hivyo, na kupata ufanisi mkubwa. Wakati huohuo, urafiki kati ya pande hizo mbili pia umeimarika.
Wakati China ilipokabiliwa na mlipuko wa virusi vya Corona, zaidi ya viongozi 50 wa nchi za Afrika walitoa salamu ama kuunga mkono juhudi za China katika kupambana na virusi hivyo. Aidha, nchi za Afrika pia zilitoa misaada halisi ikiwemo barakoa kwa China.
Baada ya virusi hivyo kulipuka barani Afrika, China imetoa misaada ya vifaa mbalimbali vya matibabu ikiwemo barakoa, mavazi na miwani ya kujilinda dhidi ya virusi, na pia vifaa vya kupumua kwa nchi za bara hilo. Balozi wa China nchini Botswana Zhao Yanbo anasema,
"Mfuko wa Jack Ma umetoa misaada mara tatu kwa Botswana, wakati huohuo, serikali kuu na serikali ya mkoa wa Shandong ya China pia zimetoa msaada wa vifaa vya matibabu kwa nchi hii. Licha ya hayo, ubalozi wa China, na Wachina walioko nchini humu pia wametoa misaada inayohitajika sana na nchi hiyo katika kukabiliana na virusi vya Corona."
China pia imebadilishana uzoefu wake wa kupambana na virusi hivyo na nchi za Afrika, na kupeleka madaktari na wataalam wa afya katika nchi hizo. Kwa mfano, tarehe 8 mwezi huu, timu ya wataalam kutoka China ilimaliza kazi ya msaada nchini Guinea Ikweta ambayo iliendelea kwa wiki mbili. Katika siku hizo wataalam hao walitembelea idara za serikali, hospitali na vituo vya upimaji, ili kubadilishana uzoefu na maofisa na madaktari wa nchi hiyo. Aidha, wataalam hao pia walitunga vitabu viwili vinavyoeleza jinsi ya kukabiliana na virusi vya Corona.
Ushirikiano na China pia umepongezwa na watu wa hali mbalimbali nchini Ghana. Balozi wa China nchini humo Wang Shiting anasema,
"Watu wa Ghana wameona ukweli, uhalisi, wema na udhati wa China kwa nchi yao. Hivi sasa kutoka serikali hadi raia wa Ghana, wote wametambua kuwa kupitia ushirikiano wa kukabiliana na virusi vya Corona, urafiki na ushirikiano kati ya nchi hizo vimeimarika zaidi."
Baada ya kutokea kwa kesi za maambukizi ya virusi vya Corona mwanzoni mwa mwezi Machi nchini Burkina Faso, China imetoa uungaji mkono wenye nguvu kubwa na kwa wakati kwa nchi hiyo. Balozi wa China nchini humo Li Jian anasema,
"Vyombo vya habari vya Burkina Faso vimetoa tahariri vikisema, China kuzisaidia nchi za Afrika kukabiliana na virusi vya Corona kunaonesha kuwa, uzoefu na ufanisi wa China unaleta matumaini mapya kwa dunia, na pia kumesaidia nchi zinazoendelea kuongeza uwezo wa kukabiliana na virusi hivyo."
Kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona, mawasiliano ya moja kwa moja kati ya China na Afrika yamepungua, na uwekezaji na biashara pia vimeathiriwa. Hata hivyo mabalozi wa China barani Afrika wamesema, baada ya kushinda virusi hivyo, biashara na ushirikiano kati ya pande hizo mbili katika sekta mbalimbali vitapata maendeleo makubwa zaidi.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |