Huzuni ya wachezaji wa Bayern Munich kushangilia ubingwa wa Ligi Kuu ya Ujerumani msimu huu bila uwepo wa mashabiki, jana ilipoozwa na kilevi cha pombe muda mfupi baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Werder Bremen. Kutokana na zuio la mashabiki kutoingia viwanjani kwa ajili ya kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya Corona, nyota wa Bayern Munich walilazimika kufanya sherehe katika vyumba vya kubadilishia nguo ambazo ziliambatana na unywaji wa pombe kwa kundi kubwa la wachezaji hao. Nyota hao wa Bayern Munich, walifanya shangwe hizo huku wakiwa wamevaa fulana na kofia maalum zilizoandikwa namba nane (8) zikimaanisha kitendo cha timu yao kutwaa taji la nane mfululizo la Bundesliga. Lakini licha ya kukosekana kwa mashabiki, kabla wachezaji hao hawajaingia vyumbani kufanya sherehe, walijikusanya pamoja na kwenda kusimama mbele ya majukwaa yaliyokuwa matupu na kushangilia kwa kupiga makofi na kupunga mikono ikiwa ni ishara ya shukrani na heshima kwa mashabiki wao. Bao pekee lililowapa ushindi Bayern katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Weserstadion lilipachikwa na mshambuliaji wao nyota, Robert Lewandoswski katika dakika ya 43. Kwa kufunga bao hilo, Lewandowski amejiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa kiatu cha ufungaji bora wa Ligi Kuu ya Ujerumani msimu huu likimfanya afikishe mabao 31. Bayern imetwaa ubingwa huo rasmi baada ya kufikisha jumla ya pointi 76 ambazo hazitoweza kufikiwa na timu yoyote ile. Kwa kutwaa ubingwa huo, Bayern inakuwa timu ya kwanza kufanya hivyo mara baada ya janga la virusi vya Corona. Nao wachezaji wa Napoli walisherehekea kutwaa taji la Coppa Italia baada ya ushindi wa penalti 4-2 kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Juventus usiku wa Jumatano Uwanja wa Olimpico Jijini Roma kufuatia sare ya 0-0. Paulo Dybala na Danilo walikosa penalti kwa upande wa Juve, wakati Napoli walifunga penalti zao zote nne za mwanzo kumpa kocha Gennaro Gattuso taji la kwanza baada ya kuwa kocha wa timu hiyo
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |