Wataalam na maofisa wa afya barani Afrika wameona kuwa uzoefu ambao China umepata katika kudhibiti na kuzuia kuenea kwa virusi vya Corona una maana kubwa na kuzitia moyo nchi za Afrika katika kupambana na janga hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la Tiba kwa Afya Njema la nchini Zambia Quince Mwabu amesema, kutokana na uzoefu wake, China ni nchi bora zaidi kusaidia nchi nyingine kupambana na virusi vya Corona. Amesema China ni nchi inayofaa kusaidia nchi nyingine kuhusu ilivyofanikiwa kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo kwa kuwa ina uzoefu, na ameongeza kuwa ni muhimu kwa nchi nyingine kushirikiana kwa karibu na China. Mwabu amesema hayo wakati wito wa ushirikiano na mshikamano kati ya Afrika na China ukitolewa katika Mkutano Maalum wa kupambana na COVID-19 uliofanyika hivi karibuni kwa njia ya video.
Naye mwenyekiti wa Shirikisho la Maendeleo ya Sekta Binafsi nchini Zambia Yusuf Dodia amesema, nchi za Afrika zinapaswa kutumia vizuri fursa hiyo ili kuhakikisha kuwa zinapata uzoefu bora zaidi kutoka China, na kwamba uzoefu wa China unapaswa kuigwa na nchi za Afrika. Dodia amesema, kuna taarifa nyingi zisizo sahihi kuhusu janga hilo, na kuongeza kuwa mataifa ya Afrika yanapaswa kuchukua nafasi kupata taarifa sahihi na pia kuanzisha ushirikiano thabiti na China.
Kwa upande wake, mkurugenzi wa Kituo cha Elimu ya China kilichoko Abuja, Nigeria, Charles Onunaiju, amesema, jambo muhimu katika mkutano wa ushirikiano na mshikamano kati ya China na Afrika katika kupambana na virusi vya Corona, linahusiana na majibu ya jamii ya kimataifa kuhusu janga hili. Mkurugenzi huyo amesema, China imepata uzoefu mkubwa katika kukabiliana na mlipuko huo, na viongozi wamebadilishana uzoefu wa mifumo ya kukabiliana na mlipuko huo, na ameeleza imani yake kuhusu mafanikio mazuri ya ushirikiano katika kupambana kwa pamoja dhidi ya janga hilo.
Nchini Zimbabwe, Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa nchini humo Sibusiso Moyo amesema, Zimbabwe iko tayari kujifunza kutoka China uzoefu wake katika kupambana na janga hilo. Amesema wangependa kubadilishana taarifa na China na nchi nyingine za Afrika, hususan kuhusu jinsi ya kudhibiti maambukizi yanayotokana na wasafiri wanaorejea nchini humo ama abiria wanaounganisha usafiri kuelekea nchi nyingine.
Katika Mkutano Maalum wa kupambana na COVID-19 uliofanyika jumatano wiki hii, rais Xi Jinping wa China aliyeongoza mkutano huo aliahidi kuendelea kuziunga mkono nchi za Afrika kwa kutoa vifaa na kupeleka timu za wataalam.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |