Nembo ya namba tatu iliyopo katika jezi mpya za Chelsea, zinaweza kutafsiriwa kama ni mkosi baada ya timu hiyo kuchapwa mabao 3-2 na West Ham ikizitumia kwa mara ya kwanza juzi. Jezi hizo mpya ambazo zitatumiwa na Chelsea msimu ujao, zina nembo ya namba tatu ambayo ni ya kampuni ya Three UK inayojihusisha na utengenezaji wa simu huko Uingereza. Kampuni hiyo ya Three UK ndio itakuwa mdhamini mpya mkuu katika jezi ya Chelsea baada ya mkataba baina ya klabu hiyo na kampuni ya matairi ya Yokohama kumalizika mwezi uliopita. Timu hiyo ilianza kuzivaa jezi hizo kwa mara ya kwanza, juzi kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya West Ham lakini ikajikuta ikipokea kichapo cha mabao 3-2 ambacho kinahatarisha uwezekano wao wa kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Katika mchezo wa jana, Chelsea licha ya kutoka nyuma na kusawazisha mabao mawili, ilijikuta ikifungwa bao la dakika za lala salama ambalo liliipa ushindi West Ham. West Ham ilipata mabao yake kupitia kwa Soucek, Michail Antonio na Andriy Yarmolenko wakati mabao mawili ya Chelsea kwenye mechi hiyo yakipachikwa na Willian. Matokeo hayo yanaifanya Chelsea inayoshika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England, kuwa mbele ya Manchester United waliopo nafasi ya tano kwa utofauti wa pointi mbili tu. Baada ya mchezo huo kocha wa Chelsea, Frank Lampard amesema wachezaji wake walimuangusha kwa asilimia kubwa.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |