MAREKANI YAJIONDOA KWENYE USHIRIKIANO NA WHO.
Rais Donald Trump hatimaye ametoa notisi ya kujiondoa kwa Marekani katika shirika la Afya Duniani WHO.
Rais huyo aliweka wazi lengo lake mwezi Mei , akililaumu shirika hilo la WHO kuwa chini ya udhibiti wa China kufuatia mlipuko wa virusi vya corona.
Licha ya wito kutoka kwa Muungano wa Ulaya na wengine, alisema kwamba ataiondoa Marekani kutoka katika kitengo hicho cha UMoja wa Mataifa UN na kupeleka ufadhili wake kwengineko.
Kufikia sasa ametoa ilani kwa UN na bunge la Congress kuhusu malengo yake, ijapokuwa mkakati huo unaweza kuchukua kipindi cha mwaka mmoja.
Stephane Dujarric, msemaji wa katibu mkuu wa UN, alithibitisha kwamba Marekani imetoa ilani kuhusu kujindoa kwake kuanzia tarehe 6 Julai 2021.
Joe Biden, ambaye atampinga rais Donald Trump katika uchaguzi wa mwezi Novemba , alituma ujumbe wa Twitter akisema: Katika siku yake ya kwanza kama rais, atairudisha Marekani katika WHO na kuimarisha uongozi wa Marekani duniani.
Marekani ndio mfadhili mkuu wa shirika hilo, likitoa $400m (£324m; €360m) mwaka 2019, takriban asilimia 15% ya bajeti yake kwa jumla.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |