Huduma ya usafiri wa abiria kwa reli ya SGR kati ya Nairobi na Mombasa zimeanza tena rasmi baada ya kusitishwa kwa zaidi ya miezi mitatu.
Treni ya kwanza iliyobeba abiria 482, ilifunga safari saa mbili asubuhi ya leo kuelekea Mombasa kutoka Nairobi. Kutokana na mlipuko wa virusi vya Corona, reli ya SGR ya Kenya kati ya Mombasa na Nairobi ilisimamisha huduma kuanzia Aprili 7. Baada ya shughuli za uchumi kufunguliwa, jana reli hiyo ianza tena kutoa huduma. Kwa mujibu wa maagizo ya serikali ya Kenya, treni zinaruhusiwa kubeba abiria kwa nusu ya uwezo wake. Mkurugenzi wa kampuni ya uendeshaji wa reli ya Afrika Star Bw. Li Jiuping amesema,
"Kutokana na maagizo ya serikali, tumefanya maandalizi ya kutosha, tunafanya upimaji kwa abiria kabla ya kuingia stesheni, na kuua vijidudu katika chumba cha kusubiria. Kwenye jukwaa la kusubiria treni, abiria wanatakiwa kuingia kwa utaratibu, bila kusongamana. Kwenye mabehewa, tunauza tiketi nusu ya uwezo wetu. Treni hiyo ina mabehewa 13, moja kati hayo linatumika kuwaweka karantini watu wanaoshukiwa kuambukizwa virusi vya Corona. Mpaka sasa treni imejaa watu, na hata ya kesho imejaa. "
Ingawa huduma ya usafiri ilisimamishwa, treni za mizigo zilizobeba vifaa vya matibabu na vitu vinavyohitajika zimefanya kazi kubwa katika kuisadia Kenya kupambana na virusi vya Corona. Hadi kufikia tarehe 30 Juni, reli hiyo ilikuwa imesafirisha makontena laki 1.96, yakiwemo ya chakula, na vifaa vya kupambana na Corona. Vilevile, serikali ya Kenya ilitumia bandari kavu ya Naivasha kuwa kituo muhimu cha kusambaza mizigo, na kupunguza kuenea kwa virusi katika eneo la Afrika Mashariki.
Naibu meneja wa idara ya utamaduni ya kampuni hiyo Bibi Olivia Mengichi amesema,
"Hadi kufikia tarehe 30 Juni, tulisafirisha tani 806 za vifaa vya mahitaji kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona, kama dawa za kuua vijidudu, alcohol n.k. Katika kipindi hicho, serikali imepunguza usafiri wa watu katika ukanda wa kaskazini. Kutumia reli ya SGR kusafirisha makontena kwenda bandari kavu ya Naivasha, kumepunguza idadi ya madereva wa malori, hivyo kumepunguza maambukizi kati ya watu na watu katika ukanda wa Kaskazini. "
Kampuni hiyo pia inasema kurejeshwa kwa huduma ya usafiri wa abiria, kutarahisisha zaidi usafiri wa watu, kupunguza maambukizi ya virusi katika usafiri wa barabara, na kuhimiza maendeleo ya uchumi wa Kenya katika kipindi cha mapambano dhidi ya virusi vya Corona.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |