Klabu ya Bayern Munich ya Ujerumani usiku wa kuamkia leo imeshinda kwa mabao 3-0 mbele ya Lyon kwenye mchezo wa nusu fainali wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Magoli ya Bayern Munich mawili yalifungwa na Gnabry katika dakika za 18 na 33 na lile la tatu lilifungwa na mshambuliaji wao machachari Lewandowski katika dakika ya 88. Sasa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya itakuwa ni kati ya Bayern Munich dhidi ya PSG. Timu zote zinatinga fainali zikiwa zimetoka kupata matokeo yanayofanana kwenye hatua ya nusu fainali. PSG ilitinga hatua ya fainali kwa kupata ushindi wa mabao 3-0 mbele ya Leipzig ya Ujerumani, kwa hiyo ushindi kwenye mechi ya fainali utategemea nani ameamka vizuri. Ufaransa imekuwa na ukame mkubwa wa kombe la klabu bingwa barani Ulaya. Mara ya mwisho ni klabu ya Marseille ndio iliyotwaa kombe hilo mwaka 1993. Fainali ya kombe hilo itachezwa nchini Uturuki jumapili ya tarehe 23, wafaransa wakiwa na hamu kubwa ya kulichukua kombe hilo. Bayern Munich imeingia fainali za kombe hilo mara 10, na imekuwa bingwa mara tano, mara ya mwisho ikiwa ni mwaka 2013, kwa hiyo kwao fainali halitakuwa jambo kubwa sana.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |