Kampuni za ndege za Kenya zazuiwa kuingiza ndege zake Tanzania
Kampuni tatu za ndege za Kenya zimezuiwa kuingia nchini Tanzania kufuatia hatua za kudhibiti janga la korona.
Mamlaka ya safari za anga ya Tanzania imezizuwia kampuni za AirKenya, Fly540 na Safarilink Aviation zote kutoka Nairobi.
Ndege za makampuni hayo kwa kawaida huwasafirisha watalii kila siku kuelekea katika Kilimanjaro na Zanzibar.
Mkurugenzi wa TCAA, Hamza Johari amethibitisha katika mahojiano na gazeti la Citizen nchini humo. Nchi hizi mbili za Afrika Mashariki zipo kwenye mzozo wa kutokukubaliana juu ya namna zinavyokabiliana na janga la virusi vya corona.
Mwezi huu Kenya ilitoa orodha ya nchi 130 ambazo wasafiri wake hawatawekwa karantini watakapoingia nchini Kenya, Tanzania haikuwemo.
Kampuni ya ndege ya Kenya -Kenya Airways pia iliwekewa marufuku ya kuingia Tanzania baada serikali ya Kenya mapema mwezi Agosti kuiondoa katika orodha ya nchi 19 zikiwemo za Afrika mashariki, ambazo raia wake hawatalazimika kuwekwa karantini kwa siku 14 watakapoingia nchini humo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |