WHO: Si kweli, maambukizi ya corona Kenya hayajapungua.
Shirika la afya duniani WHO limetilia shaka madai ya kupungua kwa idadi ya wagonjwa wa Corona nchini Kenya katika kipindi cha wiki tatu zilizopita.
Katika taarifa yake, shirika hilo limesema kwamba kushuka kwa idadi ya wagonjwa wenye maambukizi ya corona nchini Kenya hakuonyeshi picha kamili ya maambukizi nchini humo.
Taarifa hiyo inajiri baada ya rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kupongeza juhudi za Wakenya katika makabiliano dhidi ya Covid-19 akisema kwamba taifa hilo limeanza kupunguza idadi ya maambukizi.
Rais Kenyatta alisema kwamba baada ya serikali kuweka masharti ya kukabiliana na virusi hivyo Wakenya wengi walinyimwa uhuru wao lakini juhudi hizo zimezaa matunda.
Kulingana na W.H.O, madai hayo ni kinyume na kinachoendelea, kwa kuwa kaunti nyengine zinakabiliwa na ongezeko la maambukizi. Ilisema taarifa hiyo ambayo ilitolewa siku ya Jumatatu wiki hii. Shirika hilo limesema kwamba vipimo vya Covid 19 vinavyofanyiwa watu katika maabara vimepungua nchini Kenya.
Bodi hiyo ya afya duniani pia imekosoa mipango ya kuwapima Wakenya ikisema maeneo yanayolengwa ni yale ambayo hayana hatari ya maambukizi.
Baadhi ya maabara pia zimesema kwamba zinakabiliwa na uhaba wa vifaa vya kupima mbali na vifaa vya kukusanya sampuli.
Limesema kwamba utafutaji wa watu waliokaribiana na wale walioambukizwa umepungua katika kipindi cha hivi karibuni miongoni mwa kaunti 10 zenye maambukizi ya juu ambazo zinabeba mzigo mkubwa wa ugonjwa huo.
WHO liliitahadharisha Kenya dhidi kutangaza kwamba wagongwa wa Covid-19 wamepungua nchini humo.
Huku ikiwa hizi ni ishara nzuri ambazo zinaweza kutumiwa ili kuonesha kupungua kwa maambukizi, tangazo hilo linafaa kuchukuliwa na tahadhari kubwa , ilisema WHO ikiongezea kwamba kuna umuhimu wa vipimo zaidi kufanywa katika maabara mbali na kuwasaka watu waliokaribiana na walioambukizwa.
Hatahivyo akizungumza wakati wa hotuba kwa taifa kuhusu ugonjwa huo, rais Kenyatta hatahivyo aliwaonya Wakenya dhidi ya kusherehekea mapema mafanikio hayo na badala yake kuchukua tahadhari.
Alisema kwamba idadi ya maambukizi inaanza kupungua baada ya kufikia kilele chake.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |