Mshambuliaji wa Ufaransa na Paris Saint-Germain Kylian Mbappé amegunduliwa kuwa na virusi vya Corona na anatarajiwa kukosa mechi ya Ligi ya Mataifa dhidi ya Croatia inayochezwa leo. Taarifa iliyotolewa na shirikisho la soka la Ufaransa limetangaza kuwa katika vipimo alivyofanyiwa jana asubuhi yameonyesha kuwa ameambukizwa virusi vya ugonjwa huo, na baada ya hapo alitengwa na kikosi na kulazimika kurudi nyumbani. Kumekuwa na wasiwasi kuhusu ni lini na wapi aliambukizwa virusi hivyo, kwani kabla ya kujiunga na kikosi hicho, na kabla ya mchezo wa Jumamosi dhidi ya Sweden, ambapo alifunga bao la ushindi alitajwa kuwa salama. Kwenye mechi hiyo Mbappe hakuonekana kuwa fit kwa asilimia 100, na baadhi ya wachambuzi wanasema hii ni kutokana na kuumia. Kama kwenye mechi hiyo alikuwa na virusi basi ina maana wachezaji wote waliocheza kwenye mechi hiyo walikuwa kwenye hatari. Mbappé anakuwa mchezaji wa saba wa PSG kukutwa na virusi vya Corona, siku chache baada ya nyota mwingine wa PSG Neymar Junior kukumbwa na virusi hivyo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |