Serikali ya Burundi imeihakikishia Jumuiya ya Afrika mashariki kuwa nchi yao iko salama na inawakaribisha wawekezaji katika sekta mbalimbali kwenda kufanya biashara na nchi hiyo ambayo imekuwa katika machafuko ya kisiasa na kikabila kwa zaidi ya muongo mmoja.
Hayo yamebainishwa na Rais wa Burundi, Everiste Ndayishimiye, alipoitembelea Tanzania kwa ziara ya siku moja ambapo alikutana na Rais wa Tanzania, John Magufuli katika mji wa Kigoma magharibi mwa Tanzania.
Rais Ndayishimiye amebainisha kuwa baada ya kumalizika uchaguzi uliofanyika kidemokrasia, serikali yake ilikaa na pande zote za kisiasa na kukubaliana kuhakikisha nchi haiendelezi migogoro, sambamba na kufuta dhana za makabila ya watutsi na wahutu na kukubaliana kuwa Burundi ina kabila moja tu ambalo ni warundi.
Rais Magufuli amebainisha kuwa Tanzania imekubaliana na Burundi kujenga mtambo wa kisasa wa kuchenjua madini pamoja na Burundi kuuza madini yake katika soko la madini la mkoani Kigoma.
Tanzania imetaja pia kuanzishwa kwa miradi ya kimkakati kujenga reli ya kisasa kutoka Uvinza hadi Gitega, Burundi, kuboresha usafiri katika ziwa Tanganyika kwa kununua meli mpya mbili na kukarabati meli kongwe ya MV Liemba yenye umri wa zaidi ya miaka 100.
Hii ilikuwa ziara ya kwanza ya rais Ndayishimiye nje ya nchi tangu alipoapishwa kuwa rais wa jamhuri ya Burundi mwezi Julai mwaka 2020.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |