Hadi sasa China imetuma vikosi 24 vya kulinda amani vyenye wanajeshi wapatao elfu tano nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), na kutoa mchango mkubwa katika kulinda amani na utulivu wa kikanda. Wakati Sikukuu ya Taifa ya China inapokaribia, kikundi cha pili cha kikosi cha 23 cha askari wa uhandisi cha kulinda amani cha China nchini DRC kimekamilisha kazi ya kupokezana zamu na kiko tayari kurudi nyumbani China.
Kikosi cha 23 cha askari wa uhandisi cha kulinda amani cha China kilianza kutekeleza majukumu kwenye vituo vitatu nchini DRC mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka jana. Katika mwaka mmoja uliopita, wanajeshi wa kikosi hicho walikamilisha miradi 53 ya uhandisi, kuteketeza silaha 1,700 za aina mbalimbali zisizotumika, na kufanya operesheni 10 za misaada ya kibinadamu, kazi ambazo zimepongezwa na kusifiwa na Tume ya Umoja wa Mataifa nchini DRC, serikali ya DRC na watu wa nchi hiyo, na wanajeshi wote wa kikosi hicho walitunukiwa Nishani ya Amani ya Umoja wa Mataifa. Kamanda wa kikosi hicho Bw. Hou Yong anasema,
"Wakati wa janga la virusi vya Corona, tumeendelea kutekeleza majukumu ya kulinda amani katika vituo vyetu. Nishani ya Amani ya Umoja wa Mataifa ni sifa kubwa kwetu, ni heshima na pia ni msukumo."
Mwezi Desemba mwaka jana, mapigano yaliibuka ghafla na wakimbizi wa ndani wapatao elfu mbili walihamishiwa kwenye eneo la Kavumu. Kutokana na kuharibika vibaya kwa barabara pekee ya kuingia na kutoka eneo hilo, ilikuwa ni vigumu kufikisha msaada wa chakula na dawa kwa watu wenye mahitaji. Kikosi hicho cha askari wa uhandisi cha China kilitumia siku nne tu kukamilisha ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita nne, kazi ambayo ilisifiwa sana na serikali na wakimbizi wa huko.
Katika mwaka mmoja uliopita, kikosi hicho pia kilijitolea kushiriki kwenye kazi mbalimbali za kibinadamu, ikiwemo kutoa msaada wa vifaa vya elimu na michezo kwa shule tatu za msingi na Nyumba ya Watoto, na kuzisaidia taasisi hizo kusafisha mazingira, kukarabati miundombinu na kunyunyiza dawa za kuulia vijidudu. Kamanda wa kikosi hicho Bw. Hou Yong amesema:
"Katika mwaka mmoja uliopita, siku zote tumefuata mwongozo wa kulinda amani na kueneza urafiki, kukumbuka mioyoni majukumu yetu na kushikilia kanuni za usalama, na tulionesha uwajibikaji wa jeshi la China kwenye maeneo tunakotekeleza majukumu ya kulinda amani. Wakati tunapokaribia kupokezana zamu na kurudi China, tunawatakia kila la heri na mafanikio wenzetu wanaotekeleza majukumu kwenye maeneo mbalimbali nchini DRC."
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |