Bingwa wa Olimpiki katika mbio za mita 1,500 Faith Kipyegon atakuwa akifukuzia ushindi wake wa nne kwenye mashindano ya Wanda Diamond League msimu huu atakaposhiriki mbio za mita 800 kwenye duru ya Doha, Qatar mnamo Septemba 25, 2020. Kipyegon, 26, alishiriki mbio za mita 1,000 (dakika 2:29.32) jijini Monaco, Ufaransa mnamo Agosti 14 kabla ya kuandikisha muda wa dakika 2:29.92 katika mbio hizi za mizunguko miwili na nusu jijini Brussels, Ubelgiji mnamo Septemba 4. Katika duru hizo, Kipyegon alikuwa pua na mdomo kuvunja rekodi ya dunia ya dakika 2:28.98 iliyowekwa na Mrusi Svetlana Masterkova katika mbio za mita 1,000 mnamo 1996. Alirejea kushiriki fani aliyoizoea ya mita 1,500 jijini Ostrava kwenye Riadha za Dunia za Continental Gold Tour zilizoandaliwa katika uwanja wa Mestky, Jamhuri ya Czech mnamo Septemba 8. Alikosa mshindani wa kumtoa jasho katika mbio hizo alizozikamilisha kwa muda wa dakika 3:59.05 na kufuta rekodi ya dakika 4:00.96 iliyowekwa na raia wa Ethiopia Gudaf Tsegay mnamo 2017. Japo Kipyegon anapigiwa upatu wa kuwika jijini Doha, atakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Wakenya Emily Cherotich na Eunice Sum ambaye ni bingwa wa zamani wa dunia katika mbio za mita 800. Mbio hizo za mizunguko miwili zimevutia pia Winnie Nanyondo wa Uganda, Mwethiopia Alemu Habitam na Angelika Cichocka wa Poland.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |