Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amewataka wananchi wasiogope kuingia ubia na wawekezaji watakaohitaji kuwekeza miradi ya maendeleo nchini ili kuendeleza maeneo yao.
Alieleza hayo jana wakati akifungua jengo la maduka ya kisasa la Sheikh Thabit Kombo linalomilikiwa kwa ubia baina ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) na Chama cha Mapinduzi kupitia Maskani ya Kisonge, hafla iliyofanyika uwanja wa kumbukumbu ya miaka 50 ya Mapinduzi, Michenzani, Zanzibar.
Alisema kuingia ubia katika biashara ni moja ya hatua muhimu za mageuzi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Alisema mfumo huo iwapo utatumika kwa usahihi na kufuata taratibu, utaongeza kasi ya maendeleo ya nchi na kuongeza mafanikio sambamba na kuleta maslahi endelevu katika pande zilizokubaliana.
Aidha alisema utekelezaji wa mradi huo ni moja ya hatua muhimu ya kudumisha historia pamoja na kupanua wigo na fursa nyengine mpya za kiuchumi kwa Zanzibar na wananchi wake.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |