Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) limetoa orodha ya watimkaji 54 watakaoshiriki majaribio ya mbio za Kip Keino Classic mnamo Septemba 26 kabla ya Riadha hizo za Dunia kuandaliwa rasmi Oktoba 3, 2020 uwanjani Nyayo, Nairobi. Naibu Rais wa AK, Paul Mutwii, amesema majaribio ya mbio hizo wikendi hii yatajumuisha vitengo vya mita 200, mita 400 na mita 800 kwa upande wa wanaume na wanawake, mbio za kupokezana vijiti za 4×400 zitakazoshirikisha wanawake na wanaume (mixed relay) na urukaji mbali kwa upande wa wanawake.
Nia kuu ya mbio hizo ni kufanyia majaribio vifaa mbalimbali vitakavyotumiwa wakati wa Riadha za Kip Keino Classic. Rais wa Shirikisho la Riadha la Kenya (AK), Jackson Tuwei, amefichua mfumo uliotumiwa kuteua kikosi kitakachowakilisha Kenya kwenye Kip Keino Classic Tour Oktoba 3. Kwa mujibu wa Tuwei, AK ilitegemea pakubwa matokeo yaliyosajiliwa na watimkaji mbalimbali wa Kenya katika fani zao kwenye Riadha za Dunia za 2019 nchini Qatar, Michezo ya Afrika iliyofanyika jijini Rabat, Morocco na mashindano ya kitaifa. Tuwei amesema walitumia mapambano hayo kuteua kikosi cha Kip Keino Classi baada ya janga la corona kuwazuia kuandaa mchujo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |