Wananchi wa kijiji cha Chongoleani wilayani Tanga waliopitiwa na mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta linalotokea Uganda hadi Tanzania kupitia maeneo mbalimbali nchini humo jana walikabidhiwa hundi zao za malipo ya fidia kiasi cha shilingi bilioni 3.2 na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela.
Tukio la kukabidhiana hundi hizo lilifanyika katika jengo la mkuu wa Mkoa ambapo kulifanyika kikao na kuwakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa mkoa, wilaya, halmashauri, wakuu wa idara na taasisi pamoja na wananchi na viongozi wa kijiji cha Chongoleani.
Kabla ya makabidhiano hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mafuta la Taifa, James Mataragio alisema kuwa shirika limepewa dhamana ya kuhakikisha linatoa huduma za mafuta kwa wananchi kwa ukaribu hivyo wanahakikisha wanatimiza lengo lililokusudiwa kwa kuwakaribia wananchi na kutoa huduma hiyo.
Mataragio alieleza kwamba wakati wa mchakato wa kutafuta eneo la kuweka mradi huo jumla ya watu 395 walikubali kuhama na kupisha ujenzi huo na kwamba TPDC imekabidhi kiasi hicho cha fedha kwa mkuu wa mkoa kwa ajili ya malipo ya fidia zao.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |