Kampuni ya Ufaransa inayojihusisha na mafuta Rubis imetumia shilingi bilioni 2.4 kuboresha vituo vyake vya mafuta vinavyoendeshwa nchini Kenya Kenol Kobil na Gulf Energy. Fedha hizo zitatumiwa katika kuboresha vifaa katika vituo vya mafuta ifikapo mwaka wa 2020 huku ikiweka mikakati ya vituo hivyo vyote kuendesha shughuli kwa nembo ya Rubis.Katibu mkuu mtendaji wa Rubis nchini Kenya Jean-Christian Bergeron amesema gharama ya kuboresha kwa nembo kituo kimoja ni kati ya shilingi milioni 3.2 hadi 8.6.
Rubis pia imesema inalenga kujenga vituo vingine vipya vya mafuta ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kushindania soko. Rubis ilinunua vituo vya KenolKobil na Gulf energy hatua ambayo imeiweka kwenye daraja la juu la ushindani wa soko katika sekta ya mafuta nchini Kenya. Washindani wakubwa wa Rubis hivi sasa ni Total Kenya na Vivo energy Kenya. Hata hivyo Rubis imeongeza kuwa operesheni zake nchini Kenya ziliathiriwa kwa kiwango kikubwa na marufuku ya kutotoka nje iliyowekwa na serikali ili kuzuia kuenea kwa virusi vya corona. Imesema kusitishwa kwa safari za kimataifa kati ya Machi hadi Julai mwaka huu zilisababisha mahitaji ya bidhaa za mafuta kwenda chini.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |