Licha ya kuwa mwanamke wa kwanza raia wa Kenya kuwahi kujitwalia nishani kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola, Christine Ongare bado hajaweka wazi mustakabali wake kwenye ulingo wa ndondi ila amefichua azma ya kufanya hivyo baada ya Olimpiki. Ongare aliduwaza wengi kwa kujinyakulia medali ya shaba kwenye mashindano ya Jumuiya ya Madola jijini Gold Coast, Australia mnamo 2018 na akapata umaarufu zaidi alipojikatia tiketi ya kushiriki michuano ya Tokyo, Japan iliyoashirishwa kutoka 2020 hadi 2021 kwa sababu ya corona. Licha ya kwamba Olimpiki za Tokyo ziliahirishwa na kuratibiwa upya mwakani, Ongare amesisitiza kwamba hana presha ya kuingia katika usajili wa kikosi chochote cha ughaibuni kwa minajili ya kushiriki ndondi za kulipwa kwa wakati huu. Ongare kwa sasa hujifanyia mazoezi katika ukumbi wa Avefitness, eneo la Lavington, Nairobi na analenga kupata kikosi cha cha nchini Kenya kitakachoshiriki kwenye mazoezi kikilenga kunogesha Olimpiki za Tokyo. Ongare alijikatia tiketi ya Olimpiki kwa kumchapa Catherine Nanziri wa Uganda kwenye mchujo wa uzani wa flyweight (kilo 51) jijini Dakar, Senegal. Idadi ya washiriki wa kiume kwenye uzani wa flyweight katika Olimpiki za Tokyo, Japan ilipunguzwa kutoka 10 hadi wanane huku ile ya wanawake ikiongezwa kutoka watatu hadi watano.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |