Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF), Wakili Kichere Mwita Waissaka amesema kuwa suala la mchezaji wa Simba, Bernard Morrison lililowasilishwa kwenye kamati hiyo halijasikilizwa kwa kuwa mchezaji huyo alituma wawakilishi. Waissaka amesema kuwa yapo mambo ambayo yanapaswa kuwakilishwa na wawakilishi lakini kwenye suala la Morrison ambalo ni la kimaadili alipaswa awepo yeye mwenyewe ili aweze kuyajibu maswali mengine ambayo hayawezwi kujibiwa na wawakilishi. Morrison yupo kwenye mvutano na Klabu yake ya Yanga kwenye suala la mkataba wake ambapo Yanga waajiri wake wa zamani wanaeleza kuwa alikuwa na mkataba wa miaka miwili huku yeye akidai kuwa alikuwa na kandarasi ya miezi sita. Sakata hilo lilisikilizwa TFF na aliweza kushinda kwa kile kilichoelezwa kuwa mkataba ulikuwa na mapungufu kati yake na waajiri wake jambo lililomfanya awe huru kuchagua timu anayokwenda kuitumikia. Kutokana na majibu hayo Yanga walieleza kuwa wanakwenda Cas kukata rufaa ili kupata haki juu ya mchezaji huyo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |