Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku wilayani Chunya mkoani Mbeya (CHUTCU), kimesema msimu wa kilimo uliopita hali ya uzalishaji ilishuka kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa hasa mvua kunyesha kupita kiasi.
Meneja Mkuu wa CHUTCU, Juma Mohamed, amesema kuwa asilimia kubwa ya tumbaku iliyozalishwa ilikosa ubora kutokana na mvua nyingi iliyonyesha, hivyo kusababisha wananchi kushindwa kuanika zao hilo.
Alisema katika msimu wa kilimo wa 2018/19 mahitaji yalikuwa kuzalisha tani milioni 9.92, lakini uzalishaji ulipungua na kufikia tani milioni sita.
Mohamed alisema msimu uliopita wakulima walipata hasara kubwa sana kwa sababu walitumia gharama kubwa kuzalisha hususan ununuzi wa pembejeo za kilimo kama mbolea ambazo zilisombwa na maji na wengine waliovuna walishindwa kuanika.
Aidha, alisema kuwa kwa kipindi hicho bei ya tumbaku ilipungua kutoka Dola 1.6 mpaka Dola 1.33 na kwamba hali hiyo ilitokana na tatizo la kupungua ubora na uzito wa tumbaku hususan kushuka kwa soko.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |