Mtafiti wa Mazao ya Nafaka wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) Kituo cha Uyole jijini Mbeya, Dk. Denis Tippe, amewataka Watanzania kutumia uji wa ulezi ili kumaliza tatizo la udumavu kwa watoto.
Dk. Tippe amesema uji huo una virutubisho na madini mengi, yakiwamo ya zinki, ambavyo vinasaidia kukabiliana na udumavu.
Alisema mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini inaongoza kwa uzalishaji wa vyakula, lakini inaongoza kwa udumavu wa watoto kutokana na utamaduni wa wananchi kwenye ulaji ambao hauzingatii chakula bora.
Alisema uji wa ulezi ndiyo utakuwa suluhisho la tatizo hilo ikiwa wananchi wakiutumia pamoja na vyakula vingine vinavyotokana na ulezi.
Dk. Tippe alisema mikoa hiyo ni miongoni mwa mikoa ambayo zao la ulezi linastawi vizuri na hivyo akasisitiza hakuna sababu kuendelea kukabiliwa na tatizo la udumavu.
Alisema mbali na vyakula vitokanavyo na ulezi kusaidia kukabiliana na udumavu, pia vinawasaidia watu wanaougua ugonjwa wa kisukari kwa maelezo kuwa ni miongoni mwa vyakula ambavyo mmeng'enyo wake unachukua muda mrefu tofauti na mazao mengine.
Pia, alisema uji wa ulezi una madini ya chuma ambayo yanasaidia kuimarisha mifupa na meno na hivyo kusaidia watu kuwa na mifupa imara na kutong'oka meno mapema.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |