Mwenyekiti wa Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) Tawi la Nairobi, Bw. Barnaba Korir amewataka wanariadha wa Kenya kuongoza shughuli za uhamasishaji kuhusu umuhimu wa kuepuka matumizi ya dawa za kusisimua misuli michezoni. Rai ya Bw. Korir inatolewa siku chache baada ya mwanariadha Daniel Wanjiru aliyeibuka bingwa wa London Marathon mnamo 2017, kupigwa marufuku ya miaka minne kwa hatia ya kutumia dawa haramu za kusisimua misuli. Pendekezo hilo limeungwa mkono na mshikilizi wa zamani wa rekodi ya dunia katika marathon, Patrick Makau ambaye amesisitiza kwamba Kenya iko katika hatari ya kupigwa marufuku kwenye ulingo wa riadha iwapo matumizi ya dawa hizo yatakithiri. Waziri wa Michezo, Amina Mohamed amesema Serikali inapanga kupitisha sheria itakayoshuhudia wanamichezo wanaotumia dawa za hizo wakiadhibiwa vikali kwa kiwango sawa na wahalifu wengine wanaofungwa jela kwa makosa ya jinai.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |