Mgombea urais nchini Tanzania, Dk. John Magufuli (CCM), ameahidi kufufua viwanda vilivyokufa mkoani Kilimanjaro akichaguliwa tena kuendelea kuwa rais wa nchi hiyo katika uchaguzi mkuu wa tarehe 28 oktoba.
Vilevile, amewaahidi vijana wa Manispaa ya Moshi ajira za kutosha zitakazotokana na kufufuliwa kwa viwanda hivyo, akitolea mfano kuanza kwa kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Karanga.
Alitoa ahadi hiyo jana kwenye Uwanja wa Chuo cha Ushirika wilayani Moshi wakati akiomba kura kwa wananchi na wanachama wa CCM waliojitokeza kumsikiliza.
Dk. Magufuli alisema katika utekelezaji huo, serikali imeanza kukifufua kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Karanga kinachomilikiwa na Jeshi la Magereza na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).
Kwa upande wake,Mgombea urais, Tundu Lissu (CHADEMA), amesema Watanzania wakimpa ridhaa ya kuongoza nchi, atahakikisha anaimarisha uchumi kwa kuondoa sheria kandamizi na kutengeneza miundombinu mizuri kwa wafanyabiashara.
Akizungumza na wananchi wa majimbo ya Bumbuli, Korogwe Mjini, Korogwe Vijijini, Muheza na Tanga mkoani Tanga jana, Lissu alisema akichaguliwa, atahakikisha anaimarisha uchumi wa watu ili kuwa na taifa lenye watu wenye uchumi mkubwa.
Alisema akiingia madarakani, atafuta vitambulisho vya mjasiriamali vinavyotolewa na serikali kwa wafanyabiashara wadogo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |