Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetangaza kuanza kutumia stempu za kodi za kielektroniki (ETS) katika bidhaa za juisi za matunda na mbogamboga, maji ya kunywa yaliyofungashwa kwenye chupa na bidhaa za filamu na muziki yaani kanda zilizorekodiwa.
ETS zitaanza kutumika katika bidhaa hizo kuanzia Novemba Mosi, 2020 huku ikiwataka wazalishaji wote wenye leseni, waingizaji waliosajiliwa, wasambazaji, wauzaji wa bidhaa zinazotozwa kodi ya ushuru wa bidhaa kuzingatia hilo.
Kamishna Mkuu wa TRA, Dk Edwin Mhede amesema hatua hiyo inafuatia kukamilika na kuanza kwa matumizi ya mfumo huo kwa awamu ya kwanza na pili.
Awamu hizo zilihusisha bidhaa za sigara, mvinyo, pombe kali, bia, na aina zote za vileo mnamo Januari, 2019 na kwa bidhaa za vinywaji laini ilikuwa Agosti 14, 2019.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |