URA kutatua mizozo ya kodi nje ya mahakama
(GMT+08:00) 2020-10-23 18:55:48
Mamlaka ya kodi nchini Uganda URA imeamua kusuluhisho mzozo wa kodi nje ya mahakama ili kukomboa jumla ya shilingi trilioni 1.6 ambazo zimekwama kutokana na kesi nyingi mahakamani. Kamishna wa mamlaka hiyo Bi Patience Tumusiime amesema mamlaka hiyo inapanga kutafuta njia nzuri zaidi ya kutatatua migogoro ya kodi badala ya kufuata njia ya mahakama.
Ameongeza kuwa wakati nchi inaendelea kupambana na janga la corona, ni muhimu kwa mamlaka hiyo kuwaelewa wateja wao ambao hivi sasa wameathiriwa sana na janga hilo. Tumusiime ameongeza kuwa kuna baadhi ya kesi ambazo zimekaa mahakamani kwa zaidi ya miaka kumi jambo ambalo linaifanya mamlaka hiyo kushindwa kufikia kiwango cha makusanyo walichoweka.
Amesema katika bajeti ya mwaka huu wanatakiwa kukusanya jumla ya shilingi trilioni 19.6 ili kufadhili miradi ya serikali mwaka huu. Pia amewaomba wateja ambao hawajaridhishwa na hesabu zao za kodi kulipa asilimia 30 kabla ya kuwasilisha kesi mahakamani.