Katika kuunga mkono juhudi za taifa za kukuza uchumi wa bluu, Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimepanga kuanza kutoa kozi za ujenzi na utengenezaji wa meli.
Kozi hiyo maalumu katika kukuza uchumi wa bluu ama 'Blue economy' inatarajiwa kuanza kutolewa chuoni hapo kwa ngazi ya astashahada katika mwaka huu wa masomo wa 2020/21.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Chuo hicho Mabibo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Chuo Profesa Zacharia Mganilwa amesema kuwa "Uchumi wa bluu ni muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa na ustawi wa nchi, ndiyo maana baada ya kuliona hilo Chuo kimeamua kuanza kutoa kozi hiyo muhimu kwa mwaka huu wa masomo".
Profesa Mganilwa alisema pia, mbali na kuanzisha programu hiyo ya astashahada katika ujenzi na utengenezaji wa meli, Chuo kitaanzisha shahada ya kwanza ya Usimamizi na Usafirishaji katika Bandari (BSPLM). Profesa Mganilwa amewataka wazazi na vijana wa Kitanzania kuchangamkia fursa hii ya mafunzo kwa sababu sekta ya uchukuzi inakuwa kwa kasi na ina uhitaji mkubwa wa rasilimali watu hivyo kusoma kozi hizi watajitengenezea mazingira mazuri ya kupata ajira na kujiajiri.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |