Aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ya Jamhuri ya Ireland, Mick McCarthy ameteuliwa kuwa mkufunzi wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Cyprus, APOEL Nicosia kwa mkataba unaotarajiwa kutamatika rasmi mnamo Mei 2022. McCarthy, 61, amewahi pia kudhibiti mikoba ya vikosi vya Wolves na Ipswich. Aliagana rasmi na timu ya taifa ya Ireland mnamo Aprili 2020.
McCarthy alihudhuria mchuano wa APOEL dhidi ya Apollon mnamo Novemba 1, 2020 kabla ya kupokezwa rasmi mikoba ya kikosi hicho mnamo Novemba 2, 2020. Msaidizi wake, Terry Connor, aliwahi kufanya naye kazi katika kikosi cha Wolves, Ipswich na timu ya taifa ya Jamhuri ya Ireland. Ingawa APOEL ndicho kikosi kinachojivunia ufanisi mkubwa zaidi katika historia ya soka ya Cyprus, kimeanza kampeni za msimu huu vibaya na kwa sasa wanashikilia nafasi ya 10 kwa alama tisa pekee kutokana na mechi nane zilizopita. Rekodi ya mechi nne bila kusajili ushindi wowote ilikuwa kiini cha kocha raia wa Ugiriki, Marinos Ouzounidis ambaye ni kocha wa 12 wa APOEL tangu 2015. Mechi ya kwanza ya McCarthy ni kibarua cha Ligi Kuu kitakachowakutanisha APOEL na Ethnikos Achna wanaokokota nanga mkiani mwa msimamo wa ligi.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |