Kocha Pep Guardiola wa Manchester City amewataka vinara wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kurejesha kanuni mpya ya kuruhusu jumla ya wachezaji watano wa akiba kuwajibishwa katika mchuano mmoja. Kwa mujibu wa Guardiola, mrundiko wa mechi ulioshuhudiwa mwishoni mwa msimu uliopita wa 2019-20 umefanya wachezaji wengi wakipata majeraha mabaya. Vikosi vingi vya EPL vilipiga kura ya kukataa kuidhinishwa kwa kanuni hiyo ya kuchezeshwa kwa wanasoka watano wa akiba katika mechi moja msimu huu wa 2020-21. Sheria hiyo iliyopendekezwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) ilianza kutekelezwa wakati soka ya EPL iliporejeshwa mnamo Juni 2020 baada ya kusitishwa kwa zaidi ya miezi mitatu kutokana na janga la corona. Katika msimu huu, EPL ilirejea mfumo wa zamani unaoruhusu kila kikosi kufanya hadi mabadiliko matatu pekee katika mchuano mmoja. Maoni ya Guardiola yameungwa mkono na kocha Ole Gunnar Solskjaer wa Manchester United, Frank Lampard wa Chelsea na Carlo Ancelotti wa Everton.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |