Kinda wa Real Madrid Rodrygo ameiokoa klabu yake kutopata sare kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa katika hatua ya makundi ambao ulimalizika kwa Madrid kushinda mabao 3-2 dhidi ya Inter Milan ikiwa Uwanja wa nyumbani Alfredo Di Stefano. Real Madrid ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa mshambuliaji wake Karim Benzema aliyeingia kambani dakika ya 25, kabla ya Sergio Ramos kutupia bao la pili dakika ya 33, Lakini Inter ilianza kusawazisha kupitia kwa straika ambaye anawindwa sana na Barcelona dakika ya 35 naye Ivan Peresic akatupia bao la pili dakika ya 68 kipindi cha pili. Mchezo uliendelea kwa kosa kosa za hapa na pale na dakika ya 80 Rodrygo akaipatia Madrid bao la ushindi na kuifanya iondoke na alama tatu muhumu zinazoipandisha hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi B, ambapo kinara ni Borussia Monchengladbach inayoongoza kwa alama tano baada ya kushinda mechi moja na kutoka sare mbili. Madrid ambayo imekuwa na kiwango cha kupanda na kushuka tokea kuanza kwa msimu huu, katika michuano hiyo imeshinda mechi moja, ikafungwa moja na kutoka sare moja kiujumla ikiwa na alama nne. Inter ndio inashikilia mkia kwenye kundi hilo ikiwa haijashinda mchezo hata mmoja na katika michezo yake mitatu hadi sasa imetoka sare mbili na kupoteza mmoja.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |