Serikali ya kaunti ya Kiambu nchini Kenya imezindua mradi wa ujenzi wa barabara ya kilomita 75 itakayojengwa na kampuni ya H-Young. Wenyeji wa eneo la Juja katika kaunti hiyo wamepongeza hatua hiyo wakisema utawawezesha kupata mafanikio mengi ya kiuchumi. Katibu katika Wizara ya Uchukuzi Bw Paul Maringa akiwa eneo la Juja amesema barabara hiyo itagharimu takribani Sh3.9 bilioni na inaendelea kwa mfululizo bila shughuli hiyo kusitishwa.
Alisema barabara ya umbali wa kilomita 35 kuelekea Gatuanyaga pia itaunganishwa na hiyo ya Gatundu.
Alifafanua kwamba barabara hiyo inajengwa na Halmashauri ya Ujenzi wa Barabara za Mashinani (KeRRA).
Inatarajiwa kuwa ya kiwango cha kisasa ambapo itapanuliwa iwe kubwa ili magari makubwa yaweze kupita hapo.
Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro, ambaye pia aliandamana na katibu huyo kwa uzinduzi alipongeza serikali kwa kuwajali wakazi wa Juja ambao kwa muda mrefu wamekuwa na shida ya usafiri.
Nyoro alisema baada ya barabara hiyo kukamilika umeme utasambazwa ili kurahisisha biashara na kupunguza uhalifu.
Aliwahimiza wahandisi wanaoendesha mradi huo kuhakikisha vijana walio katika maeneo hayo wanapewa nafasi ya kwanza kupata ajira.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |