• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China kuipa kipaumbele Afrika katika utoaji wa chanjo ya covid-19

    (GMT+08:00) 2020-11-12 10:40:38

    Serikali ya China imeapa kuipa Kenya, watu wake na Afrika kwa ujumla kipaumbele pindi tu itakapopata chanjo ya ugonjwa wa COVID-19. Balozi wa China nchini Kenya Bwana Zhou Pingjian alibainisha kuwa utawala wa Rais Xi Jinping utaendelea kusimama na nchi zinazoendelea, hasa barani Afrika, katika juhudi zinazolenga kushinda janga hilo ambalo limesababisha mateso kwa binadamu pamoja na mgogoro mkubwa zaidi wa kiuchumi na kijamii.

    Akizungumza baada ya mkutano na kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga, Zhou alisisitiza ahadi ya nchi yake "kuchukua uongozi katika kutafuta chanjo salama na yenye ufanisi katika kutibu COVID-19 na kuitoa kwa bei nafuu pamoja na kuhakikisha inapatikana kote Afrika", ofa iliyokaribishwa na kiongozi huyo wa Chama cha Orange Democratic Movement.

    "Tunataka kuishukuru serikali ya China kwa ahadi yake ya kuhakikisha kuwa pindi chanjo itakapokuwa tayari, itapatikana kwa urahisi na kwa bei nafuu barani Afrika," Raila alisema.

    Tayari chanjo ya COVID-19 iliyotengenezwa na kampuni ya China National Biotech Group (CNBG) iko katika hatua za mwisho za majaribio katika nchi kadhaa ikiwa ni pamoja na baadhi ya mataifa barani Afrika ikiwemo Morroco.

    Watafiti wameonyesha imani yao katika chanjo hiyo ambayo wanasema ni salama kwani tayari imeidhinishwa katika mpango wa dharura nchini China inayowalenga wafanyakazi muhimu na wengine walio katika hatari kubwa ya maambukizi.

    Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani WHO, kati ya chanjo kumi za virusi vya corona ambazo zimeendelea hadi kufikia majaribio ya awamu ya tatu duniani, nne zinatengenezwa na wanasayansi wa China.

    Ahadi hiyo imetolewa sambamba na ile iliyotolewa baada ya mkutano wa hivi karibuni kati ya Rais wa China na viongozi wa Afrika akiwemo Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, ambapo Beijing ilisisitiza umuhimu wa ushirikiano, na kutoa wito wa umoja, mshikamano na juhudi za pamoja za kukabiliana na janga hilo, huku usaidizi mkubwa ukitakiwa kuelekezewa hasa kwa watu walio katika mazingira magumu.

    Mara baada ya mtu wa kwanza mwenye corona kuripotiwa barani Afrika, China ilichukua hatua za haraka, na kuhamasisha utoaji wa rasilimali kusaidia mapambano dhidi ya ugonjwa huo. Serikali na makampuni binafsi ya China kama vile Alibaba, yalitoa mavazi ya kinga, barakoa, na dawa kwa karibu kila taifa barani humo.

    Wakati wa mkutano huo na Odinga, Aidha, Balozi Zhou aliahidi kuwa serikali yake inaunga mkono zaidi maendeleo ya viwanda vya Kenya, sambamba na wito wa Bw. Odinga wa kuzingatia uzalishaji zaidi.

    Wakati huo huo, Odinga alitoa wito wa ushirikiano wa kimataifa katika kushughulikia mambo yanayoikumba dunia, ikiwa ni pamoja na janga la COVID-19 na mabadiliko ya hali ya hewa.

    Pia aliomba China kuongeza msaada wake kwenye maendeleo ya miundombinu nchini Kenya na Afrika.

    Wawili hao pia walijadili masuala mengine ya ndani ambayo kwa sasa yanasababisha gumzo kwa umma ikiwa ni pamoja na mpango wa maridhiano maarufu BBI ambapo Odinga alitoa taarifa kuhusu hatua ambazo zimepigwa hadi sasa katika mchakato wa kudumisha mshikamano na umoja wa Wakenya.

    "Odinga alitumia fursa hiyo kuelezea mambo muhimu ya ripoti ya kamati kuhusu utekelezaji wa maridhiano na ujenzi wa taifa la Kenya." Taarifa kutoka kwa msemaji wa Raila, Dennis Onyango ilisema

    Picha:

    Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga na balozi wa China nchini Kenya Bwana Zhou Pingjian wakiwa katika ofisi ya Odinga ya Capitol Hill jijini Nairobi. PICHA/KWA HISANI

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako