Aliyekuwa mtendaji Mkuu wa klabu ya Simba ambaye kwa sasa yupo ndani ya kampuni inayoidhamini Klabu ya Yanga (GSM) kama mshauri kuelekea mfumo mpya wa uendeshaji wa klabu hiyo, Senzo Mazingisa, jana alishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa muda kabla ya kuachiwa. Mapema jana taarifa za kukamatwa kwa Senzo zilianza kusambaa mchana kwenye mitandao ya kijamii zikimhusisha na tuhuma za upangaji matokeo kwenye baadhi ya michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara. Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alipotafutwa kuthibitisha kushikiliwa kwa Senzo alielekeza kutafutwa Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kinondoni. Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM, Injinia Hersi Saidi, alisema yeye hayupo kwenye nafasi ya kuelezea jambo hilo. Hata hivyo Msemaji wa Klabu ya Yanga, Hassan Bumbuli alikiri kuwa Senzo alishikiliwa na Polisi, lakini aliachiwa jana hiyo hiyo baada ya kutoa maelezo yake.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |