Wakati timu ya Simba ikiwa ni miongoni mwa klabu zinazojiandaa na michuano ya Ligi ya Mabingwa, Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), limeongeza idadi ya wachezaji wanaoweza kuzitumikia klabu zinazoshiriki michuano yake yote kutoka 30 hadi 40. Simba itaifuata Plateau United ya Nigeria kwenye mechi ya awali ya hatua ya mtoano itakayochezwa kati ya Novemba 27-29 kabla ya kurudiana katika mechi ya nyumbani kati ya Desemba 4-6. Katika tarehe hizo Namungo itaanzia nyumbani dhidi ya Al Rabita FC ya Sudan kwenye Kombe la Shirikisho Afrika. Hatua hiyo imefikiwa kutokana na miongozo ya itifaki za afya za FIFA na CAF dhidi ya COVID-19 na kwa kuelekea kuanza tena kwa mashindano, wachezaji wanaopimwa na kubainika kuwa na virusi vya corona hawaruhusiwi kushiriki kwenye mechi. Kamati ya Dharura ya CAF, imeruhusu timu tofauti zinazoshiriki mashindano ya shirikisho hilo kuwa na idadi ya kutosha ya wachezaji wa kucheza mechi, na imepitisha hatua hiyo kutokana na mapendekezo ya Kamati ya Maandalizi ya AFCON iliyofikia uamuzi huo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |