Serikali ya Kenya kupitia uongozi wa ngome ya Fort Jesus mjini Mombasa imeanza kushirikiana na kampuni ya kutoa huduma za kiteknolojia n a kampuni ya Jays Pyrotechnics Ltd kufanya maonyesho ya historia ya ngome hiyo. Maonyesho hayo ni pamoja na utengenezaji wa filamu na picha ikiwa ni njia ya kuelezea historia ya ngome hiyo ya kitalii. Mkurugenzi mkuu wa Jays Pyrotechnics Ltd, Bi Jayshree Suchak, amesema kwa muda wa miaka 10 hivi wanatazamia kupata mapato ya Sh20 bilioni kutoka kwa mradi huo. Uongozi wa Fort Jesus umesema fedha hizo zitatumiwa kukarabati ngome hiyo na mji wa Old Town ili kuirejeshea hadhi yake ya zamani. Alisema kuwa tayari mradi huo wa kutengeneza picha na kutumia teknolojia kuelezea matukio ya kale umewagharimu Sh150 milioni na uliwachukua muda wa miaka miwili toka 2018 hadi 2020.
Utafiti na utengenezaji wa filamu na picha hizo ulifanywa na Wakenya. Picha hizo zinaonyeshwa katika ukuta mmoja wa ngome hiyo kupitia teknolojia ya sasa maarufu kama "Augmented Reality".
Bi Suchak alisema mradi huo utawasaidia kueleza Wakenya na wageni kuhusu historia ya ngome hiyo yenye umri wa zaidi ya miaka 400. Waziri wa Michezo na Turathi za Kitaifa wa Kenya Bi Amina Mohamed amesema hatua hiyo itachangia zaidi kupiga jeki sekta ya utalii ambayo imeathiriwa pakubwa na janga la corona. Amina ameongeza kuwa katika eneo la Pwani, kuna maeneo tofauti ya kihistoria kama vile mnara wa Vasco Da Gama, mabaki ya Gedi Ruins na mengineyo ambayo bado yanahitaji kuhifadhiwa kwa manufaa ya watalii.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |