Ni utamadauni wa kufana, ambao umekuwepo kwa vizazi vingi na bado ni maarufu miongoni mwa watu wa China. Utamaduni wa okestra ya jadi kwa kichina huheshimiwa na wengi, vijana kwa wazee pamoja. Lakini kinachofanya uwe wa kipekee, ni jinsi ulivyo na mvuto kwa watu. Mengi yamesemwa kuhusu utamaduni huu, lakini ukibahatika kujionea mwenyewe maonyesho yake, ndio unaweza kuelewa zaidi.
Lengo lake, ni kukuza na kuendeleza urithi wa muziki wa China na utamaduni wake halisi. Lakini kuna nia nyingine ambayo ni zaidi ya lengo hilo. Maonyesho ya sanaa hii yanawakutanisha wachina na kuwafanya wawe na mshikamano. Baadhi ya mashabiki wamebaini kuwa, sanaa hii inawaunganisha katika azma ya kujenga utaifa, na kuhimiza uzalendo.
Katika siku moja ya maonyesho, kukindi cha sanaa cha jeshi la China, kiliongoza matumbuizo, huku wasikilizaji wakitumia fursa hii kutafakari historia ya nchi, na hata mambo yajayo.
Nyimbo kama vile "Hakutakuwa na China mpya bila chama cha kikomunisti", "Vita vitakatifu", "Kwaheri mama", "Leo ni siku yako ya kuzaliwa China" na "China tukufu", zilnawafanya mashabiki kuwa na furaha kubwa. Kwa wakati mmoja wakati bendi la jeshi ikiendelea kutumbuiza, mashabiki walijipata wakitoa machozi ya furaha, hasa kutokana na ustadi usio wa kawaida.
Lakini kuna jambo fulani lililonivutia. Nilipodurusu historia ya wanamuziki hao wa bedi ya jeshi la China PLA, niligundua ni kwa nini ilikuwa rahisi kwao kutumbuiza kwa umahiri. Kila msanii alikuwa na wasifu wa kipekee. Wasanii hao wote wana tuzo za kitaifa na kimataifa baada ya miaka mingi ya kazi ya usanii.
Katika tovuti yake, kundi hili linasema "daima linasisitiza hisia za watu wa kawaida katika muziki wake." Lakini mbali hayo, ofisa mmoja wa China Africa Press Center, CAPC mjini Beijing, alinieleza kuwa "katika mwanzo wa uzinduzi wa taifa la China, nchi hii haikuwa na mawasiliano ya kiutamaduni na nchi za nje.
"Wakati huo, China haikuwa imeanzisha soko la utamaduni kwa kuzingatia idadi kubwa ya watu wake, na wataalam wa mziki kufanya kazi kwa ajili yake." Alisema afisa huyo
Hii labda ni pengo ambalo kundi hili la Okestra ya PLA pamoja na makundi mbalimbali ya opera nchini China wamekuja kujaza, kwa kusaidiwa na Wizara ya Utamaduni, na katika mchakato wa kuwaongoza wafuasi na kuvutia mamia ya mashabiki wengi vijana. Nilipokuwa nikiwaza siku moja baadaye, nilitambua kuwa tamasha hii ni moja ya njia za kujenga na kudumisha umoja kwa Wachina. Nikahisi kuwa labda taifa lenye jamii mbalimbali linaweza kukuza mshikamano na ushirikiano kupitia njia kama hii. Naelewa kuna njia mbalimbali za kuafikia ndoto hii, lakini hii inaweza tu kuwa njia nyingine moja ya kufanya hivyo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |