• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Kuondoa mkanganyo wa tiba ya jadi ya kichina

    (GMT+08:00) 2017-03-27 20:02:41

    Sehemu kubwa ya maisha ya watu wa China yakini ni ya kipekee na tofauti ikilinganishwa na mataifa mengine duniani. Mfumo wa afya katika taifa la China ni mojawapo. Tofauti na aina nyingine za dawa za jadi ambazo kwa kiasi kikubwa yaonekana kutokomea, tiba asilia ya Kichina maarufu TCM inaendelea kunawiri.

    Hakuna anayeweza kukana kwamba tiba hii ya jadi bila shaka ni maarufu zaidi na imekukubaliwa na wengi katika siku za kisasa nchini China. Ni moja ya mambo ya msingi ya dunia ya kale na huheshimiwa. Aina hii ya tiba hata hivyo si ya wachina pekee kwani imepata umaarufu katika maeneo mengine ya dunia.

    Maarufu jinsi ilivyo, wakosoaji wengi wamehoji ufanisi wake katika kutoa ufumbuzi wa afya. Kwa kweli, walio na shaka, wengi wao kutoka nchi za magharibi, ufikiria ni udanganyifu unaotokana na siku za rais wa kwanza wa Jamhuri ya watu wa China, bwana Mao Zedong.

    Wao wanadai kuwa Rais Mao, maarufu kama Mwenyekiti Mao, alipiga tarumbeta kuhusu aina hii ya dawa ili kutafuta njia ya kuhuunganisha kwenye siku ya kisasa ya jamii ili kuinua ukuaji wa kiuchumi katika sekta ya dawa Beijing.

    Kwenye hoja zao, uchambuzi wa sumu wa dawa zake haufanyiki kwenye maabara na kuongeza uwezekano mkubwa wa maadhara.

    Mimi hivi karibuni nilizuru Jimbo la Jiangsu na kutembelea hospitali moja katika mji wa Nanjing nikiwa na lengo maalum katika idara ya tiba asilia ya Kichina, ili kubainisha ukweli na usahihi wa taarifa hizi.

    Nilikutana na Profesa Sun Jian Hua, ambaye ni daktari na mkurugenzi katika idara hiyo. Kabla ya mimi kudadizi zaidi kuhusu ufanisi wa aina hii ya matibabu, alikuwa mwepesi kusema kuwa "kuna ongezeko kubwa la mahitaji ya mfumo huu wa matibabu kwa njia ya asilia."

    Uchambuzi wangu wa haraka wa hali ya mambo ulibaini kuwa vitanda vyote hospitalini vilikuwa vimejaa wanaotafuta uuguzi huu, kando na foleni kubwa niliyoshuhudia ya wale waliokuwa wakingoja kupata dawa hizo.

    Lakini ni kwa nini idadi kubwa ya watu wakakumbatia huu utamaduni sana kama kweli hauna manufaa katika maisha yao?

    Akijibu swali hili, Profesa Sun alisema kwamba "Watu wanakuja hapa kwa idadi kubwa kwa sababu wanaamini katika utamaduni huu. Ni bora kwa kila njia na hii ni kutokana na tofauti ya mfumo wa uponyaji."

    Kutoka wakati huo yeye alitaka kurahisisha ufahamu wa tiba hii ya karne kwa karne ya jadi.

    "Wauguzi wetu kabla ya karne ya 19 walitegemea uchunguzi, majaribio na makosa. Lakini TCM imefanyiwa marekebisho mno. Wakati wa miongo miwili iliyopita tumekuwa tukifanya majaribio ya kliniki ya kuthibitisha kuwa ni zaidi ya kile watu wanadhani." Alisema

    Daktari Hellen Fu, ambaye anafanya kazi katika idara hiyo, alitoa mchango wake katika hoja ile na kufichua kuwa "kwa mara nyingi sisi tunashughulikia kesi za magonjwa ambayo yamekuwa sugu kwa dawa za kisasa."

    Akijibu maswali juu ya mafunzo ya wauguzi wa TCM, Profesa Sun alisema "madaktari wetu ni maalumu kwa maarifa. Wao wamepata mafunzo ya kitaaluma. Wanajua hasa muundo wa mwili wa binadamu."

    Anasisitiza kwamba kuitimu kuwa daktari katika tiba ya asilia ya Kichina si rahisi kama wengi wanavyodhania, akiongeza kuwa muda wa kusomea taaluma hii si chini ya miaka minane (8) katika chuo kikuu.

    "Wanafunzi ujifunza elimu ya msingi ya TCM katika chuo kikuu kwa miaka mitano. Kisha wana tarajali katika sehemu ya kliniki na lazima kupita mtihani ili kupata kufuzu kuwa daktari. tarajali huenda kwa miaka mitatu (3)." Alisema Prof Sun.

    Kulingana na yeye, tiba hii ya kale imefanyiwa mabadiliko mengi kwa miaka mingi. Mabadiliko ambayo inaweka uchunguzi wa magonjwa kuwa cha msingi.

    "Tofauti nyingi zipo kati ya aina hii tiba na dawa za magharibi. Baada ya utambuzi, tunafanya uamuzi kama ugonjwa huo unaweza kutibiwa na TCM au madawa ya magharibi. Wauguzi wetu umakinika hasa na msingi na chanzo cha ugonjwa." Prof Sun alisema.

    Tiba ya sindano (acupuncture), t'ai chi na matibabu ya mitishamba inapatika kwa vituo vingi vya afya. Hii inathibitishwa na idadi ya wagonjwa wanaopokea aina hii ya matibabu.

    Katika tiba ya sindano, kwa mfano, Prof Sun anasema madaktari wao wanajua ni wapi pa kutoboa. Yeye anesema kwamba hakuna kesi yoyote ya kifo imeripotiwa tangu, kwani madaktari wao kamwe hawapitishi sindano kupitia vyombo muhimu vya mwili kama vile mishipa, mapafu na figo. Anasisitiza kuwa wauguzi wao watambua jinsi ya kuepuka vyombo hivi kwa ukamilifu kwa sababu ya mafunzo wao upokea.

    "Tunafanya majaribio ya kliniki ambapo sisi tunawagawanya wagonjwa katika makundi mawili. Wengine wanapokea matibabu ya sindano ilhali wengine hawapokei."

    Yeye anadai kwamba utamaduni huu umepata umaarufu katika nchi nyingi duniani kwa sababu ni nafuu, akitoa mfano wa shughuli katika Kliniki ya Cleveland uko Marekani ambapo wengi uuzuru kutafuta mfumo huu wa tiba wa asilia ya Kichina.

    "Tiba hii haitumiki tu katika magonjwa, inatumika pia katika ICU (Kitengo cha wagonjwa mahututi). Majeshi sasa wanaajiri madaktari walioitimu matibabu ya sindano "acupuncture". Aidha sisi tumeendelea kutoa msaada wa matibabu kote duniani kwa njia ya mfumo huu. "Alisema.

    Waafrika hawajawachwa nyuma kwani wanafunzi kadhaa kutoka bara hilo wanajiunga na vyuo vikuu vinavyotoa mafunzo hayo hapa China. Mwenzangu Theopista Nsangugwanko alikutana na baadhi yao na ameandaa ripoti.

    Wenye shaka siku zote watakuwepo, lakini Prof Sun anasema tiba hii itaendelea kukubalika na kukumbatiwa zaidi huku akisisitiza kuwa tamaduni hii itakuwepo kwa muda mrefu.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako