• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Kampuni Maarufu ya uchapishaji ya China ya Phoenix yatafuta washirika Afrika

    (GMT+08:00) 2017-03-31 15:29:13

    Na Eric Biegon-Beijing, China.

    Kampuni maarufu ya uchapishaji kutoka China sasa inanuia kupanua shughuli zake barani Afrika kuanzia mwaka huu. Kampuni hiyo ya Phoenix Publishing Media Group imetangaza kuwa inatafuta makampuni kutoka bara hilo ili kushirikiana katika sekta ya uchapishaji.

    kampuni hiyo ambayo imesifika kwa ajili ya uchapishaji na usambazaji wa vitabu na majarida ama kwa kweli imefichua kuwa kwa muda mrefu imekuwa ikimezea mate na kutafakari kuingia soko la Afrika. Usimamizi wake hata hivyo unasema jitihada hizi zimekwamishwa na ugumu unaotokana na vibali vya kazi katika mataifa fulani barani Afrika.

    "Tumekuwa tukifanyia marekebisho shughuli ya biashara zetu kwa kujumuisha vikundi tofauti. Tungependa mfumo wa ushirikiano ambapo tuna washirika ndani ya nchi mbalimbali barani Afrika." Mkurugenzi Mtendaji na rais wa kampuni hiyo Jiankang Zhang alisema.

    kampuni hiyo hivi karibuni ilizindua kiwanda cha uchapishaji Namibia, ambapo iliweka mtambo mkubwa wa kisasa wa digitali ya uchapishaji. Hata hivyo wakuu wa kampuni hiyo wanadai kuwa hii haitoshi kwani soko la mahitaji Afrika ni kubwa mno, hali ambayo sasa imewalazimisha kupanua shughuli zake.

    "Uwepo wetu ni dhahiri katika Namibia. Lakini hatutaki kuweka kiwanda cha uchapishaji peke yake. Tunataka kuwa na wadau wa ndani Afrika kwani sisi nia yetu ni kutoa huduma zetu za uchapishaji wa hali ya juu Afrika." Bwana She Jiangtao ambaye ni naibu mtendaji mkuu wa kampuni hiyo alikariri.

    Nafasi ya kushirikiana kulingana na kampuni hiyo ni wazi kwa wote. Usimamizi huo unasema hauna vigezo maalum unaotumia kuorodhesha makampuni yenye agenda yake, bora tu ni wahusika katika sekta ya uchapishaji. Wawili hao walithibitisha kuwa kila taasisi ya umma na binafsi wako huru kutafuta mahusiano na kampuni hiyo.

    "Nataka mjue kuwa Phoenix ina nia ya kushirikiana na yeyote anayefanya kazi ya uchapishaji wa ndani tutakayefanya kazi pamoja ili kufikia malengo yetu" alisema Bw. Jiankang

    Lakini mara tu watakapodumisha ushirikiano na nchi mwenyeji, Kampuni hiyo imetangaza kuwa itasongea hatua ya pili ambapo itaanzisha matawi ya ndani.

    "Kwa sasa sisi tu tunataka kuwa na washirika wa ndani katika nchi za Afrika. Kutoka hapo tutaanza mchakato wa kuanzisha makampuni ya uchapishaji." Aliongeza bwana Jiangkang

    Wakihutubia waandishi wa habari kutoka Afrika ambao walizuru kiwanda cha uchapishaji wake iliyoko Nanjing, makao makuu ya shughuli zake, wasimamizi wa kampuni hiyo walisema kuwa upanuzi wa Phoenix kunamaanisha kuwa ni lazima kuwe na ushirikiano wa kukuza na kubadilishana utamaduni kati ya China na Afrika.

    "Sisi tungependa kutambulisha bidhaa muhimu kutoka Afrika kwenye soko la China na bidhaa za China kwa njia kama ile ile kwenye soko la Afrika. Ushirikiano wetu wa kitamaduni ni muhimu kwa ndoto hii. Kupitia ubadilishanaji huu tutambua manufaa pamoja." Alisema bwana Jiankang

    Lakini inaonekana hii haitakuwa ni mara ya kwanza ya kampuni hii kuwa na ushirikiano na Afrika. Bwana Jiankang alifichua kwamba baadhi ya wachapishaji kutoka Kenya, Ethiopia na Namibia wametafuta huduma zao siku za awali.

    "Mwaka jana (2016), sisi tumeupokea ujumbe kutoka Kenya. Walikuwa wakitafuta uchapishaji wa vitabu vya ziada. Sisi tunao uwezo huo. Tutaendelea kufanya hivyo kwa makampuni mengine yote ambayo wanahitaji ubunifu wetu". Alibainisha bwana She

    Mbali na uchapishaji na usambazaji wa vitabu, kampuni hiyo hujishughulisha katika uchapishaji wa vifaa vya biashara, usimamizi wa hoteli, uwekezaji wa fedha na biashara ya mali isiyohamishika.

    Hadi sasa kampuni ya Phoenix imekita mizizi nchini Uingereza, Marekani na Australia na kuingia kwake katika soko la Afrika itapiga jeki kwa kiasi kikubwa sekta ya uchapishaji ambayo inajitahidi kwa sasa.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako