Beijing imetangaza kuwa imeboresha ushirikiano wake na Afrika kufikia kiwango cha kina kimkakati. Hii hoja ya karibuni kulingana na maafisa wakuu wa serikali ya China itaharakisha utekelezaji wa malengo muhimu yaliyoandaliwa hasa kuwezesha mataifa ya Africa kuwa bora kiuchumi na kujitegemea.
Hatua hii hata hivyo inajiri huku China ikikiri wasiwasi wake kuhusu kile ilichotaja kuwa vikwazo vingi vinavyochipuka wakati ambayo serikali hiyo inapanua shughuli zake barani Afrika. Serikali ya China inahofia kuwa vikwazo hivi vinaweza kuhathiri uwekezaji endelevu barani humo.
Katika mwaka wa 2015, wakati wa mkutano wa ushirikiano baina ya China na Afrika uliofanyika nchini Afrika Kusini, Rais Xi Jinping alitangaza kuwa serikali yake ilitenga billioni 60 dola za marekani kutumika kwa ajili ya upanuzi wa miradi mbalimbali kwa mataifa ya Afrika.
Kutoka kapu hilo, bilioni 5 dola za Marekani zilikuwa zimetolewa kama msaada, hii ikiwa ni kutimiza lengo la kuheshimu kanuni ya usawa na manufaa ya pamoja, afisa mkuu anayehusika na mambo ya Afrika katika wizara ya kigeni alithibitisha.
Kwa mujibu wa Bwana Dai Bing, ambaye ni naibu mkurugenzi mkuu katika idara ya masuala ya Afrika katika wizara ya mambo ya nje China, billioni 35 dola za Marekani ilitolewa kama mikopo kusaidia Afrika kujenga miundombinu. Mpango huu kwa mujibu wa afisa huyo hutegemea sana manufaa yanayoafikiwa kutoka kwa miradi hizo.
Billioni 20 dola za marekani zilizosalia, zilitengwa kama akiba ya kuziwezesha na kujenga uwezo wa biashara ndogo ndogo na za kati almaarufu SME's katika Afrika miongoni mwa masuala mengine.
Hadi sasa Wizara ya biashara ya China, imethibitisha kwamba Bilioni 30 dola za Marekani tayari zilitolewa huku nusu nyingine ikiwekwa mpangilio.
Yote tisa, taifa hilo lenye uchumi mkubwa Zaidi barani Asia, inataka kuboresha ushirikiano wake na Afrika kwa hatua nyingine. Ngazi hii ya ushirikiano kwa mujibu wa China itaongozwa na masharti kali. Ni ngazi ambayo imetajwa kuwa kipindi cha "maendeleo makubwa."
"Wakati wa kuandaa rasimu ya maeneo ya ushirikiano, sisi tulifanya utafiti mkubwa ili kuelewa mahitaji ya Afrika. Tunataka kusaidia Afrika kuziba nyufa zake na kuafikia kiasi kinachohitajika kimaendeleo." Alisema bwana Dai.
Bwana Dai alithibitisha kuwa kando na maeneo kumi ya ushirikiano yaliyoratibishwa awali katika mkutano FOCAC, China imebainisha kuwa viwanda na kilimo cha kisasa ni maeneo ya msingi ambayo yatachochea ukuaji Afrika. Hata hivyo serikali hiyo iliyoko Beijing imekuwa ikianzisha miradi ya majaribio ili kubainisha hali ya baadaye ya mipango hiyo. Hadi kufikia sasa ni mataifa machache tu za Afrika zimepokea programu hizi.
"Katika hatua hii tunasisitiza miradi kuwa na majaribio ya kwanza. Kenya, Tanzania, Ethiopia na Kongo yamenufaika na programu hizi majaribio. Tutafanya miradi ya majaribio na kama tutafanikiwa, tutaweza kueneza kwa nchi zaidi. Kama tutapata vikwazo, basi itasaidia kutoa mwelekeo tutakaofuata. "Alibainisha Bw Dai
Ni hapa ambapo alithibitisha kuwa itakuwa ni vigumu kwa China kushirikiana na nchi zote katika bara la Afrika. Hata hivyo afisa huyo alikuwa mwepesi kusema kwamba miradi kutoka China zinapanuka kwa misingi ya taratibu. Sababu kuu inayochochea hatua hii alielezea, ni faida za kiuchumi yatokanayo na miradi yote yaliyoanzishwa na makampuni ya Kichina.
"Wakati tunajenga reli toka sasa kwenda mbele, tunataka kuhakikisha kama una thamani ya kiuchumi. Sisi tunahofu hatari ya kijamii na mzigo utakaowacha kwa maeneo yatakayotekelezwa. Sasa tunasisitiza kuhusu faida za kiuchumi na kijamii. "Alisema.
Mazingira hafifu ya uwekezaji Afrika
Kwa mara ya kwanza, idara ya masuala kuhusu Afrika imezungumzia kile kilichotaja kuwa hali mbaya ambayo makampuni ya Kichina zinalazimika kuvumilia katika jitihada zao kuwekeza katika Afrika. Kwa mujibu wa Bw Dai, mazingara ya uwekezaji katika sehemu nyingi za Afrika bado ni duni.
"Sheria na kanuni juu ya uwekezaji wa kigeni inakosekana katika baadhi ya mataifa. Hakuna hakikisho ya kisheria. Hakuna ulinzi kwa uwekezaji huu. Makampuni yetu hujisikia kusita kufanya kazi." Alisema bwana Dai.
Lakini hii ni moja tu katika orodha ya vikwazo Beijing imerekodi hadi sasa. Dai anafichua kuwa idadi kubwa ya nchi bado zinaimiza ulinzi wa soko, na hii imepunguza biashara huru. Hii ikiwa ni pamoja na kodi kubwa inayotozwa ambayo wakati mwingine inaathiri faida baada ya uwekezaji.
Zaidi ya hayo, Dai alikariri kuwa ukosefu wa ufanisi katika taratibu za kibiashara umefanya mambo kuwa magumu zaidi. Alifichua kuwa mchakato ambao kwa kawaida huchukua wiki 2 tu katika China na nchi nyingine, huenda ukachukua muda wa miezi 3 hadi 6 katika idadi kubwa ya mataifa ya Afrika.
"Afrika inahitaji marekebisho ya taratibu na kuzirahisisha. Hakuna haja ya kutafuta usaidizi katika idara mbalimbali za serikali, kwa mfano. Haya yote yanaweza kufanyika chini ya paa moja. Kuna haja ya kuongeza utendakazi bora." Dai alisisitiza.
Lakini labda kile kinachoonekana kutishia uwekezaji zaidi Afrika kutoka mataifa ya nje ni swala la kushindwa kwa baadhi ya serikali za Afrika kuwekeza katika mahitaji muhimu zinazohitajika katika miundombinu ambazo tayari zimekamilika.
"Vifaa kama barabara, umeme na maji zimebaki hali duni katika hali nyingi. Tunajenga viwanja na barabara katika baadhi ya nchi, lakini serikali zimeshindwa na ugavi wa maji na umeme. Mifereji ya takataka pamoja na barabara zimeziba na kusababisha mijengo hii kuwa katika hali mbaya."Alilalala bwana Dai
Alisema hali hii ya kuathirika kwa miradi mingi zilizoanzishwa na makampuni ya Kichina si ya kuridhisha, lakini hata zaidi, imechangia kuharibu sifa nzuri ya baadhi ya makampuni ya China yaliyo bora duniani.
Ukosefu wa usalama bado ni changamoto kubwa inayoathiri uwekezaji Afrika kwani bwana Dai anasema China imepoteza idadi kubwa ya wafanyakazi waliotumwa Afrika kwa sababu ya vurugu, akiongelea kesi ya hivi karibuni katika moja ya nchi, ambapo walinzi watatu wa mradi unaoendelea waliuawa kikatili.
Anasema serikali za Afrika lazima zifanye sehemu yao ya kusaidia makampuni ya kigeni wanaotaka kuwekeza katika maeneo yao wakati China inaendelea kupanua uwekezaji katika bara hilo.
"Tunapaswa kuambiana ukweli na uhalisia wa mambo. Kuaminiana na kusaidiana. China haitafuti maslahi yake ya kibinafsi na kipekee katika ushirikiano wetu na Afrika." Bwana Dai alisema.
Serikali ya China inadumisha kuwa itatimiza ahadi zake zote kwa bara hilo lakini inatoa wito kwa serikali za Afrika zilizoathirika na hali hii pia kuheshimu na kutimiza mapatano yaliyowekwa.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |