• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Wanawake Afrika kutimiza ndoto zao kwa kutumia pendekezo la Ukanda Mmoja na Njia Moja

    (GMT+08:00) 2017-06-09 13:05:26
    Na THEOPISTA NSANZUGWANKO, BEIJING

    IKIWA ni wiki chache tangu kufanyika kwa kongamano la kwanza kuhusu Mkanda Mmoja Njia Moja mjini hapa wanawake kutoka nchi mbalimbali za Afrika kwa kushirikiana na wenzao kutoka China wameandaa tamasha kuangalia namna ya kujikwamua katika kujiletea maendeleo.

    Katika Tamasha hilo lililoshirikisha wanawake zaidi ya 100, wameweza kujadili namna ya kutumia pendekezo la Ukanda mmoja njia moja kwa wanawake kupeleka maendeleo katika nchi zao za Afrika.

    Muandaaji wa Tamasha hilo, Angelina Makoye ambaye ni mwanafunzi wa mahusiano ya Kibiashara nchini China akitokea Tanzania anaweka bayana kuwa lengo hasa ni kuhakikisha wanawake wa Afrika walioko nchini China wanatumia fursa ya Pendekezo hilo ipasavyo.

    Pia kwa kutumia fursa zilizopo nchini China, watatoa elimu kwa wanawake katika kujenga mazingira ya kuondokana na umasikini na kukuza uchumi wa mwanamke.

    "Katika tamasha hili,ni mwanzo wa kutimiza ndoto yangu ya kila siku kuhakikisha wanawake na wasichana wa Afrika wanapata nafasi ya kukaa na kujadili namna ya kumuwezesha mwanamke na kupata ushauri,hasa kwa wasichana waliopo vyuoni nchini humu "alisema.

    Anaeleza kuwa tangu mkutano wa wanawake duniani wa mwaka 1995 hakuna nchi duniani iliyotekeleza mikakati waliyokubaliana katika kukabiliana na changamoto kwa wanawake.

    Hivyo kwa wanawake waliopo nchini China na kupatiwa fursa mbalimbali kama ufadhili wa shule,kazi na nyinginezo kuhakikisha kunakuwa na mikakati ya pamoja ya kukomesha vitendo hivyo kwa kuwafikia wengi zaidi kutumia Pendekezo hilo linalosisitiza muingiliano wa watu wa mataifa mbalimbali.

    Anasema ataendelea kufanya matamasha kama hayo ili kuwafikia wasichana wengi zaidi wanosoma katika vyuo mbalimbali nchini humo kuunganisha nguvu na kuwa watekelezaji wa uwezeshaji wanawake katika Nyanja tofauti.

    Anasema kwa kutumia Pendekezo la Ukanda mmoja njia moja kutakuwa na muingiliano katika Biashara, sera mbalimbali kwa China na Afrika, ufadhili katika miradi ya wanawake kwa lengo la kuwawezesha kujiinua kiuchumi kote duniani.

    Akifungua Tamasha hilo,balozi wa Tanzania nchini China,Mbelwa Kairuki anawasihi wanawake kutoka nchi mbalimbali za Afrika kutumia pendekezo la Ukanda mmoja njia moja katika kujiletea maendeleo. Anaeleza kuwa suala ni kuhakikisha wanakuwa na mipango endelevu kwani nchi ya China imetumia pendekezo hilo kufungua milango kwa waafrika na nchi nyingine Duniani na wanawake wana nafasi kubwa ya kutumia pendekezo hilo kuondokana na unyonge walionao.

    Anaeleza kuwa kati ya wafanyabioashara wanaofanya biashara kwa kiasi kikubwa kati ya China na Afrika ni katika jimbo la Guangdong, kwenye mji wa Guangzhoe na asilimia 40 ya wafanyabiashara hao ni wanawake ambao wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kujiletea maendeleo.

    Anasema idadi ya wanawake wanaofanya biashara baina ya Afrika na China inaweza kuongezeka zaidi kwa wanawake wa pande zote kuungana katika tekelezaji wa kipaumbele Ukanda mmoja Njia moja.

    "Ukanda mmoja njia moja kwa wanawake ni fursa kubwa katika kupeleka maendeleo kwa wenngine walio Afrika kwani China katika utekelezaji wake imefanya masuala mengi kwa wanawake ikiwemo ufadhili kwa wanafunzi wa kike, pamoja na muingiliano wa watu na tamaduni zao" anasisitiza.

    Anasema katika kufikia mikakati hiyo ni vema wanawake waliko vyuoni kusoma kwa bidii, kujiamini na pale unapopata fursa ya kazi au biashara kuhakikisha inafanikiwa bila kukata tamaa huku wakiwezesha wengine walioko katika nchi za Afrika.

    Anasema ushirikiano wa nchi za Afrika na China umekuwa na mafanikio makubwa kwa wengi wao wamefanikiwa katika biashara zao za kuuza bidhaa za China na Afrika, huku katika Ukanda mmoja Njia moja China wamejenga miundombinu ya barabara ,Reli,miradi ya Umeme na mengineyo ambayo moja kwa moja ina matokeo chanya kwa wanawake wa Afrika.

    Katika tamasha hilo, wanawake maarufu nchini China kutoka Afrika walinena na wanawake hao kuwajenga katika kuhakikisha wanatimiza ndoto zao za Maendeleo wakiwa nchini China .

    Mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Beijing Information Sience and Technology ambaye ni Raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) aliyeishi Marekani,Emilia Mpwo anawataka wanawake wa Afrika waliopo nchini China kutumia Ufadhili wa masomo unaotolewa kujiendeleza.

    "Mimi ni mwalimu ,na nina miaka inakaribia 60 lakini niko shule nikichukua masomo yangua ya PHD, hivyo inabidi kujiendeleza kwa kutumia ufadhili unaotolewa na China kwa wanawake katika vyuo mbalimbali" anasema.

    Anaeleza jinsi alivyopata shida kusoma huku akifanya kazi nchini Marekani na kutaka fursa za China kutumika kwa maendeleo ya wanawake hao na nchi za Afrika kwa Ujumla.

    Naye mnenaji kutoka nchini Nigeria,Gloria Okolo anaeleza mazingira yanayoweza kuwafanya wanawake kufikia ndoto zao kuwa makini na watu wanaowazunguka katika kuwaleza ndoto hizo katika kufikia malengo.

    "Umakini unatakiwa katika kuchagua mtu wa kumwambia ndoto zako kwani wapo hata ndugu wa karibu au marafiki watakaokukatisha tamaa kwa sababu zao hivyo ni vema kuwa makini kwa kumsikiliza anavyopokea ndoto zako na ukimuona anakukatisha tamaa ni vema kuachana naye" anasema.

    Tamasha hilo lililofanyiliwa na Kampuni za nchini China za gazeti ya China Daily ya China,Startime, pia Kampuni ya magazeti ya Serikali (TSN) ya nchini Tanzania ikiwa pekee toka Tanzania iliyodhamini.

    TSN ni wachapishaji wa magazeti ya Serikali ya Daily News, Sunday News, Habarileo Jumapili na Sport Leo, imefadhili kutokana na ujumbe mzito kwa tamasha hilo kwa wanawake wa Afrika ikiwemo Tanzania kutumia fursa ya nchini China.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako