Na Theopista Nsanzugwanko- Beijing, China.
KATIKA kukabiliana na vitendo vya uhalifu duniani,China imehaidi kutoa misaada zaidi wa kifedha na rasilimali mbalimbali kusaidia jamii ya kimataifa kupambana na changamoto za kiusalama duniani.
Hatua hiyo ya China imetokana na kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu duniani hasa Ugaidi,uhalifu wa kitandao na uhalifu mwingine unaoathiri dunia na kusababisha hofu ya usalama duniani katika kuleta maendeleo.
Akizungumza wakati anafungua Mkutano mkuu wa 86 wa taasisi ya usalama Duniani 'Interpol' mjini hapa,Rais wa China Xi Jinping anaonyesha nia yake kusaidia kupambana na usalama ulimwenguni katika miaka mitano ijayo kwa kutoa kipaumbele kwa nchi zinazoendelea hususan zile za Afrika.
" lazima nchi zote duniani kwa pamoja ziwe na mikakati endelevu katika kushirikiana kukabiliana na changamoto za kiusalama zilizopo na ili kuhakikisha linafanikiwa ni lazima mataifa makubwa duniani kusaidia mataifa madogo na yanayoendelea"anaweka wazi rais huyo wa China.
Anasema nchi hiyo ya pili kuwa na uchumi mkubwa duniani kila mwaka imekuwa na jitihada za kusaidia kukabiliana na uhalifu mkubwa duniani kama Ugaidi ,uhalifu wa kimtandao na vitendo vipya vya uhalifu vinavyoibuka duniani.
Anasema watasaidia katika kujenga uwezo uwezo katika mifumo ya mawasiliano na maabara za uchunguzi wa makosa ya jinai katika nchi 100 zinazoendelea Duniani ,nyingi zikiwa nchi kutoka Afrika.
Pia ,kwa usimamizi wa wizara ya ulinzi nchini humo,wana mikakati ya kuanzisha Chuo cha kutoa mafunzo ya kimataifa kwa wasimamizi wa sheria, kitakachotoa mafunzo kwa wataalamu 20,000 kutoka nchi zinazoendelea.
Katika kuhakikisha kunakuwa na usalama duniani,Rais huyo anaeleza kuwa China imepeleka walinzi wa amani 2,609 kusaidia ujumbe wa Umoja wa Mataifa kulinda amani katika nchi nane zilikiwemo Sudani Kusini,Mali na Liberia kutoka Afrika.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na washiriki kutoka nchi 158 duniani,Rais huyo anaeleza wazi kuwa ulinzi na usalama duniani si rahisi kwa nchi au ukanda mmoja mmoja hivyo ni lazima kuwa na mikakati ya pamoja.
Naye,Rais wa Interpol, Meng Hongwei anazungumza katika mkutano huo kuwa jukumu la taasisi hiyo kuunganisha nguvu za pamoja duniani katika kuimarisha vyombo vyote vya usalama jambo litakalosaidia kukabilia na uhalifu
Anasema licha ya kutoa misaada ya kiutaalamu ,taasisi hiyo ina kazi ya kuunganisha nguvu za vyombo vya ulinzi katika jumuiya ya kimataifa kuwa na mikakati ya pamoja katika miaka ijayo.
"Maendeleo ya kiteknolojia na utandawazi vimekuwa vikibadilisha vitendo vya uhalifu ,na kuwa uhalifu wa kimataifa jambo linalofanya kuwa ngumu kwa nchi moja kukabiliana na uhalifu wa aina mbalimbali peke yake"anasema Meng
Anasema kuanzia mwaka 2000 hadi 2006 matukio 70,000 ya ushambulizi wa kigaidi yametokea duniani na bado jamii ya kimataifa inatafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hilo.
Katika mkutano huo uliofanyika kwa siku nne mbali na kuangalia kwa undani jinsi ya kukabiliana na uhalifu wa kwenye mitandao pia walijadiliana kwa kina kuhakikisha mifumo ya mawasiliao kwa nchi zote wanachama inakuwa madhubuti kwa taasisi kusaidia nchi zenye mifumo duni.
Taasisi ya Interpol yenye makao makuu yake nchini Ufaransa sasa ina nchi wanachana 192 baada ya kupitishwa kwa nchi ya Palestina na Visiwa na Solomoni kuwa wanachama katika mkutano huo mkuu .
Mkutano huo,ulikutanisha maafisa wakuu kutoka vyombo vya ulinzi na usalama na mawaziri wanaoshughulikia usalama 1,000 katika nchi 156 na kufanikiwa kupitisha makubaliano 19.
Mkutano mkuu ujao wa 87 utafanyika Novemba mwakani katika mji wa Dubai,Nchi ya Falme za Kiarabu.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |