Na Eric Biegon jijini Beijing, China.
Serikali ya China sasa inasema itaingiza rasilimali na fedha zaidi katika miradi ya utafiti ili kuelewa mahitaji ya wananchi barani Afrika. Utawala huo wenye makao yake jijini Beijing unasema kuwa ufahamu mwafaka kuhusu bara hilo lilatoa nafasi nzuri kwa taifa hilo lenye uchumi mkubwa barani Asia kutoa mchango wake na msaada dhabiti katika jitihada zake za kusaidia hali ya maisha katika Afrika.
Makamu waziri wa mambo ya nje wa China Zhang Ming anasema serikali ya Rais Xi Jinping inakusudia kufanya hivyo kwa kushirikisha huduma ya wasomi wake walio na uelewa kuhusu bara la Afrika.
Lakini ili kuhakikisha mafanikio katika shughuli hii, wataalam hao kutoka China pia watatakiwa kufanya kazi kwa karibu na wenzao katika nchi watakaozuru barani Afrika.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa vitabu vitatu juu ya Afrika vilivyoandikwa na msomi mashuhuri wa Kichina Profesa Liu Hongwu, waziri huyo msaidizi alihoji kuwa wakati muafaka umewadia kwa Wachina kuelewa Afrika kikamilifu kwa jinsi ilivyo wala si kwa jinsi inavyosemwa. Alisema hiyo itatoa taarifa mwafaka na ya kuaminika kuhusu bara hilo ambazo zinaweza kusaidia kubadili hatima yake.
"Tunahitaji kuwa na dira ya Afrika kulingana na matokeo yetu halisi, si ya kutoka Magharibi, au Hollywood au vile wanavyosema "bara lililokata tamaa" kama wanavyoonyesha katika baadhi vyombo vya habari." Alibainisha
Zhang Ming, aliyekuwa balozi wa China nchini Kenya, anasema yeye binafsi amekuwa akiwarahi wasomi wa Kichina kufanya utafiti zaidi juu ya Afrika. Aidha aliweka wazi kwamba serikali ya China imekuwa ikiwafadhili kifedha na kutoa msaada wa kimsingi ili kufanikisha juhudi hizi.
Hata hivyo Zhang anakiri kwamba shughuli hii sio rahisi akisema ilikuwa ni vigumu kuwashawishi wasomi kuondoka nyumbani mwao kutembelea Afrika na kufanya utafiti wa nje. Lakini miaka michache baadaye, anasema hali imebadilika kutokana na kwamba kwa sasa kuna ushindani mkubwa miongoni mwa wasomi wa Kichina wanaopigania kupata nafasi hii.
Hata hivyo anaonya kwamba watafiti hao kutoka China hawatakuwa na anasa za kufanya kazi kutoka mahali popote isipokuwa katika Afrika iwapo wanataka kufanikiwa katika mradi huo.
"Sisi hatutaki watafiti wetu wafanye kazi kutoka ofisi na kufikiria kuhusu Afrika. Kuweza kuelewa Afrika ni lazima uishi na kufanya kazi huko. Hii ni njia pekee ya uhakika ya kupata matokeo imara na ya thamani." Yeye alisema.
Zhang alibainisha kuwa ushirikiano wa China na Afrika umeingia hatua ya kimkakati akisema kuwa nchi yake inataka kufanya masomo ya Afrika katika mtazamo wa macho ya Kichina, kutokana na mawasiliano ya moja kwa moja na watu wa Afrika.
"Jukumu la kubadilishana kitaaluma katika ajenda yetu ya ushirikiano ni dhahiri. Wasomi ni mojawapo ya nguzo tano za ushirikiano kati ya China na Afrika." Alisema
Aliwahamasisha wasomi wa Kichina kuwa na kiasi, na wawe tayari kujifunza kutoka Afrika na kupanua wigo wa utafiti wao.
Malengo ya China katika Afrika imekuwa wazi kwa wote kuona. Idadi inayoongezeka ya vyuo vikuu vya Kichina vinavyoanzisha idara ya mafunzo ya Afrika ni ushahidi tosha. Matokeo yamekuwa masomo mengi yaliofanywa na vitabu vingi viliyochapishwa kuhusu Afrika na wasomi wa Kichina.
Hivyo si kwa bahati mbaya kwamba mwandishi wa vitabu hivyo, Prof Liu, ni rais wa Taasisi ya Mafunzo ya Afrika katika Chuo Kikuu cha Zhejiang Normal. Waziri masaidizi Zhang alivipongeza vitabu hivyo vilivyozinduliwa akivitaja kuwa "mchanganyiko bora wa maendeleo ya nadharia na vitendo vya majaribio."
Vitabu hivyo vimeandikwa katika lugha ya Kichina na kwa wasomaji wa Kichina kwa sasa. Katika moja ya vitabu yenye jina "Kutoka China Southwest Borderland kwa Bara la Afrika", Prof Liu alitoa nyaraka kuhusu uzoefu wake katika Afrika katika miaka zaidi ya 10 aliofanya kazi na kuishi katika bara hilo kutoka nchi moja hadi nyingine.
Uzinduzi wa vitabu hivyo vipya liliandaliwa na Chama cha watu wa China kwa urafiki wa mashirika ya nje ya nchi, CPAFFC.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |