Na Theopista Nsanzugwanko,Beijing
MPANGO wa ukanda mmoja njia moja,ulioanzishwa na Rais wa China mwaka 2013 na kutenga fedha zaidi ya dola za Marekani bilioni 100 kwa lengo la kumaliza miundombinu mibovu,kufadhiri miradi mbalimbali pamoja na kusaidia maendeleo ya utaalamu katika mataifa yanayoendelea.
Mpango huo unapita katika mabara matatu ya Afrika,Ulaya na Asia ambako ndiyo nchi ya China ipo na kuanzia wakati huo nchi mbalimbali zimekuwa zikijiunga tayari kwa utekelezaji.
Katika kuhakikisha mpango huo unafanikiwa mwezi uliopita katika mkutano wa chama tawala nchini China cha CPC waliingiza mpango huo katika katiba ya chama chao kwa lengo la kutekelezwa kwa uhakika zaidi.
Kwa kutambua hilo,wiki hii viongozi kutoka nchi za Afrika wamekutana kuhamasishana nchi zaidi kujiunga na mpango wa mkanda mmoja njia moja kwa lengo la kukuza ushirikiano baina ya nchi hizo na China pamoja na kujiletea maendeleo katika Nyanja tofauti.
Viongozi kutoka katika taasisi za nchi mbalimbali zaidi 20 pamoja na mabalozi wanaowakilisha nchi za Afrika walikutana katika mkutano wa viongozi wa taasisi inayojenga urafiki kati ya China na Afrika wakiwa na kauli mbiu ya Fursa mpya zinazojitokeza katika mpango wa Ukanda mmoja na njia moja kutokana na ushirikiano wa Afrika na China.
Katika mkutano huo,pia ulishirikisha viongozi mbalimbali kutoka mikoa zaidi ya 15 ya nchini China kwa lengo la kubadilishana mawazo kuhusu nchi za Afrika na kukuza ushirikiano na mikoa hiyo katika uwekezaji,biashara na mengineyo.
Katika ufunguzi wa wa mkutano huo,viongozi wa Afrika walipongeza uamuzi wa mkutano wa 19 wa chama cha Kikomunisti cha CPC kuingiza suala la mpango huo katika katiba ya chama hicho na kusema ni mwamko mpya kwa nchi za Afrika kutumia mpango huo kwa ajili ya Maendeleo.
Katibu mkuu wa Shirikisho la kukuza urafiki kati ya Tanzania na China (TCFPA) Joseph Kahama anasema mpango huu umepokelewa Afrika kwa kukuza amani,manufaa kwa wote katika Nyanja tofauti.
Kahama anasema ili kuhakikisha mafanikio zaidi yanapatikana katika nchi za Afrika ni vema kuwa na majadiliano uwazi kuhusu changamoto katika nchi mbalimbali zinazopitiwa na mpango huo.
Anasema ni vema kuwa na ushirikiano kwa watunga sera kwa kuangalia hali ya nchi husika hasa katika biashara na uchumi kwa China na nchi nyingine za Afrika kutekeleza sera zitakazonufaisha pande zote.
""muhimu zaidi kwa China na nchi shiriki za mpango huu kuzingatia mambo muhimu kama ushirikiano wa biashara na uwekezaji kuliko kutumia muda mwingi kupambana na changamoto za kiufundi zinazotokana na sera zisizofaa"anasisitiza
Pia anasema ,mpango wa ukanda mmoja njia moja unashirikisha nchi zaidi ya 65 zenye hali tofauti katika masuala ya utamaduni na uchumi hivyo China kama msimamizi mkuu ni vema nchi washiriki kuwa na ajenga ya kutumia mpango huo kwa manufaa ya nchi zote na siyo kufanya mashindano.
Naye,Balozi wa Madagasca nchini China ,Victor Sikonina ambaye ni Mkuu wa Mabalozi wa mataifa ya Afrika nchini humo anasema mpango huo unahakikisha kukuza maendeleo ya nchi husika pamoja na kuboresha maisha ya watu.
Hivyo alizisihi nchi nyingine ambazo bado hazijajiunga na mpango huo kufanya hivyo kwa lengo la kujiletea maendeleo kwani hakuna namna ya nchi za Afriika kuuepuka mpango kama kweli wanahitaji maendeleo.
Madagasca tayari imejiunga na mpango huo mapema na sasa wanaendelea na mikakati ya utekelezaji kwa lengo la kuleta maendeleo na kukuza ushirikiano na pande hizo mbili.
Katika hotuba yake,Rais wa Shirikisho la urafiki bain ya Botswana na China,Kgosi Puso anasema kwa mpango huo inatoa nafasi ya kuelewana,kubadilishana uzoefu pamoja na mwingiliano wa watu kutoka nchi mbalimbali.
Anasema urafiki wa nchi siyo kwa wanadiplomasia pekee lakini inatakiwa kufika mpaka kwa watu wa chini hivyo mpango huo unakuza urafiki na ushirikiano baina wananchi wote.
Anasema ushirikiano katika mwamko mpya inamaanisha kuwa na mtazamo mpya katika kukabiliana na changamoto mbalimbali kwa kuzifanya kuwa fursa katika mpango wa Ukanda mmoja njia moja.
Naye,Mkurugenzi mkuuwa idara ya masuala ya afrika katika wizara ya Mambo ya nje China,Dai Bing aweka wazi kuwa mpango huo una lengo la kujenga jamii yenye usawa .
"mwingiliano wa watu katika masuala mbalimbali,pamoja na maisha bora kwa wananchi wa viwango tofauti ndiyo lengo la chama tawala nchini humo na ndiyo sababu ya mpango huo kuwekwa katika katiba ili kufikia watu wengi ikiwemo Afrika"anasema.
mwisho
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |