Ni dhahiri shairi kuwa China na Marekani zipo katika mgogoro wa kibiashara. Hali hii inahitaji majadiliano mapana na ya kina baina ya pande zote mbili.
Bila udhibiti na utatuzi wa mapema wa hali hii, ni wazi kuwa madhara yake hayatakuwa kwa China au Marekani tu, dunia nzima itapata hasara kwa namna yoyote ile.
Msingi wa hofu ya athari katika msuguano huu, unajengwa na kuegemezwa kwenye ukweli kuwa mataifa haya mawili yana nguvu kubwa na ushawishi wa hali ya juu kiuchumi.
Katika taarifa mbalimbali za Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa, nchi hizi mbili bado zinaendelea kushika nafasi za juu katika uchumi wa dunia.
China, kwa mfano, kwa mwaka jana uchangiaji wake katika ukuaji wa uchumi wa dunia ulizidi asilimia 30.
Hii inamaanisha kwamba hali yoyote itakayoathiri uchumi wake, ikiwa pia ni moja ya mataifa yenye uwekezaji mkubwa sana nje ya nchi, itaaathiri mwenendo wa biashara, uwekezaji na uchumi duniani.
Benki ya Dunia imekwishatoa muelekeo wa uchumi wa dunia kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2018, inayoonyesha kuwa hali ya upatikanaji wa fedha katika uchumi itakuwa njema.
Pamoja na tathmini hii, ni vyema suala la mgogoro wa kibiashara kati ya China na Marekani likachukuliwa kwa tahadhari kubwa, kwa sababu linaweza kubadili hali ya uchumi wa dunia.
Siku chache baada ya Rais wa Marekani Bw. Donald Trump kutangaza mpango wa Marekani kutoza ushuru mpya bidhaa kutoka China wenye thamani ya dola bilioni 60, China kwa upande wake nayo pia imetangaza hatua ya kukabiliana na hali hiyo.
Jumatatu wiki hii, China imetangaza orodha ya bidhaa 128 za Marekani zitakazotozwa ushuru, yenye thamani ya dola bilioni 3, ikiwa ni kile kinachoonekana kama ni hatua za 'kulipiza kisasi'.
Ikumbukwe kuwa vita' hii ' ni kama ya mafahari wawili wanapambana, mwisho wa siku nyasi zitaumia kwa kiasi kikubwa. Ushawishi wa haya mataifa mawili na nguvu waliyonayo kiuchumi duniani huashiria kuwa athari ya hii sintofahamu ya kibiashara haitaiacha salama dunia.
Shirika la Biashara Duniani (WTO) nayo kwa upande wake tayari limekwishaonya kuwa vikwazo hivi vipya vya kibiashara kati ya China na Marekani vitaathiri uchumi wa dunia.
Kwa kile kinachoonekana kama njia ya kidiplomasia kulipatia ufumbuzi hili tatizo, China inaendelea kuamini kuwa njia pekee ya kutatua hii hali ni kupitia njia ya majadiliano.
Hata hivyo inaonya kuwa haigopi vita ya kibiashara na iko tayari kwa namna yoyote ile kulinda maslahi yake.
Kwa nyakati tofauti, maofisa waandamizi wa serikali ya China wamejitokeza kuzungumzia juu ya mgogoro huu, huku wakionya kuwa hakutakuwa na mshindi.
Aidha wamekuwa wakionya kuwa athari zake hazitakuwa kwa mataifa hayo mawili tu, bali utakuwa na madhara kwa uchumi wa dunia kwa ujumla, na kupendekeza kuwepo kwa njia ya wazi ya majadiliano ili kuondoa tofauti hizo.
Kwa China, nchi ya pili kwa uchumi baada ya Marekani, hii hali inakuja wakati ambao wachambuzi wa uchumi wanasema siyo wakati sahihi.
Ni wakati ambao China, kwa gharama yoyote na hali yoyote iko katika jitihada za kutekeleza diplomasia ya kiuchumi kwa vitendo inayoegemea zaidi katika dhana ya usawa na kunufaishana.
Ni dhahiri kuwa hii ni mojawapo ya sababu kuu inayosukuma China kuamini kuwa kukaa mezani na kufanya majadiliano ili kufikia muafaka, ndio njia pekee na bora zaidi ya kutatua huu msuguano.
Vyombo vya habari mbalimbali duniani kwa nyakati tofauti, vimeandika na kuchambua athari za kiuchumi ambazo zinaweza kuikumba dunia siku za usoni endapo hakutakuwa na ufumbuzi wa haraka na wa kudumu wa tofauti za kibiashara kati ya China na Marekani.
Ni wakati muafaka sasa, jumuiya za kimataifa ikaingilia kati na kuyashawishi mataifa haya mawili kukaa mezani kwa nia njema kabisa ya kutafuta ufumbuzi ili kutatua changamoto hii ambayo mwisho wa siku haitakuwa na mshindi.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |