Na Eric Biegon - NAIROBI
Katika dunia nzima, mataifa yanafuatilia kwa karibu matukio yanayoendelea katika nchi mbili yenye chumi kubwa ulimwenguni ambayo huenda yakasababisha malumbano ya kibiashara kati ya Beijing na Washington.
Ama kwa kweli wengi wanatarajia mambo hayataharibika na kufikia hatua hii. Hata hivyo dalili si nzuri. Ni suala la ushuru kwa sasa, lakini kwa kiasi kikubwa vita vya biashara vinaonekana kukaribia kwa kasi.
Wakati serikali ya Rais wa Marekani Donald Trump ilitangaza ushuru wa ziada kwa bidhaa kutoka China, nchi hiyo inayotawaliwa na chama cha Kikomunisti ilijibu kwa njia sawia, kwa kutangaza ushuru zaidi kwa bidhaa za kilimo kutoka Marekani ambazo ni asilimia kubwa ya mauzo ya nje kuingia China.
Na sio hilo tu, kwani wizara ya biashara ya China ilitishia kutoza ushuru mkubwa bidhaa zaidi kutoka Marekani. Kwa kufanya hivyo, wizara hiyo ilionya kwamba ulipizaji kisasi wa hali hii ingeguza kila pembe ya Marekani.
Wachanganuzi wa masuala ya jamii kutoka mataifa ya nje wanashikilia mtazamo kwamba vita vya kibiashara kati China na Marekani haviwezi kuepukika hasa maslahi ya kimataifa ya nchi hizo mbili zinapozingatiwa.
"Huu ni mgogoro wa kawaida kati ya mamlaka kubwa duniani ya jinsi gani wanaweza kufanya biashara na kila mmoja. Ni sera ya America kwanza dhidi ya sera ya China kushinikiza utandawazi ambao unashamiri." Profesa mashuhuri wa chuo kikuu kutoka Kenya na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Macharia Munene alisema
Maslahi ndiyo, lakini tayari idadi kubwa ya raia wa Marekani wameelezea hofu yao juu ya uwezekano wa malumbano ya biashara baina yao na China, na kumtaka Rais Trump kufikiri upya hoja hii.
Wale ambao wamezungumza waziwazi juu ya suala hili wanadai kuwa Amerika haina uwezo wa kushiriki malumbano na China. Lakini ni rahisi kuona ni kwa nini.
Hadi sasa, kwa mfano, china imenunua karibu nusu ya maharage inayozalishwa Marekani. Hata sasa kuna uvumi kwamba China inaweza kuagiza bidhaa hii kutoka Brazil na Argentina. Iwapo hii itatokea, basi hatua hii itaumiza wakulima wa Marekani.
"Nafasi yangu kama mtu ambaye angependa kuwakilisha Southern Minnesota ni kwamba tunahitaji kufanya kila tuwezalo kupanua mauzo ya nje na kujenga masoko mapya kwa ajili ya bidhaa zetu." Alisema Jim Hagedorn ambaye anagombea ofisi kwa chama cha Republican katika jimbo la Minnesota wakati wa kampeni hivi karibuni.
Pia alitoa maoni yake kuhusiana na mustakabali wa biashara ya nyama nchini Marekani, hasa nyama ya nguruwe, akisema kuwa utawala wa Trump lazima iwasaidia raia kupata masoko zaidi kwa ajili ya bidhaa kote duniani.
"Natumahi Rais atafanya kila awezalo kuhakikisha wakulima wetu wana masoko ya kimataifa na hatutapata vikwazo zaidi." alisema.
Lakini kwa nini wananchi wa Marekani wana wasiwasi kuhusu malumbano ya biashara na China?
"Wamarekani watapoteza vita hivi kwa kuwa wanadaiwa zaidi ya dola trilioni 3 na China. Atakayepata hasara zaidi katika malumbano haya ni Marekani. China itashinda kwani imekuza sera ya biashara huru kwa muda mrefu."Alisema Munene
Kwanza, anasema China imeunda soko kubwa ya bidhaa zake ndani ya China na nje ya Marekani. Anasema inawezekana kuwa utawala wa China ulioko jijini Beijing imekuwa ikijiandaa kwa ajili ya nyakati kama hizi na hii inaweza kuonekana katika sera yake ya kushinikiza utandawazi.
"Masoko yanayoongezeka kwa kasi kwa ajili ya bidhaa zinazozalishwa na China, kama kompyuta mbali na simu za mkononi, yanapatikana katika mataifa yanayoendelea kama vile India, Amerika ya Kusini, na Afrika." Anasema.
Kwa upande mwingine, anasema China yenyewe ni soko kubwa kwa bidhaa za Marekani. Kwa mfano, anasema kwamba mamia ya mamilioni ya simu aina ya iphone ya Marekani yananunuliwa na watumiaji kutoka China. Na iphone ni sehemu ndogo tu ya mauzo ya nje ya Marekani.
Macharia hata hivyo ana maoni kwamba serikali ya Rais Xi Jinping ina sera ya taifa ya kukuza mageuzi na kufungua milango yake kwa dunia. Hii ndio sababu kwa maoni yake, itakuwa vigumu kwa China kufunga milango yake kwa mazungumzo na mashauriano zaidi.
Athari Africa
Lakini je, vikwazo hivi vinaweza kuwa na athari zozote barani Afrika?
Wachanganuzi wanaamini kwamba athari itagonga kila pembe ya dunia kutokana na muunganiko wa dunia. Lakini kwa sasa inaonekana Afrika haitaathirika pakubwa au kuteseka lolote kamwe kulingana na Profesa Macharia.
"Hakuna madhara ya moja kwa moja juu ya Afrika kwa kuwa bidhaa zake hazijawekewa vikwazo vyovyote vya ushuru. Kwa hiyo, hakuna uhusiano wa moja kwa moja." Alisema
Lakini China kwa sasa ni mshirika mkuu wa Afrika kibiashara. China inahusika katika uchimbaji wa rasilimali Afrika na biashara baina yao iliongezeka mara kumi katika miaka kumi ya kwanza ya karne hii.
"Mgogoro wao unahusu ni nani anayefanya biashara zaidi ya mwingine, siyo tatizo la Afrika lakini tatizo lao." Aliongeza
Kulingana na wizara ya biashara ya China, biashara kati ya Afrika na China ilifikia dola bilioni 170 mwaka 2016 ikilinganishwa na dola bilioni 50 na Marekani. Hii ndiyo sababu Macharia anaamini Afrika haiwezi kukaa vizuri ilihali mzozo unatokota baina ya China na Marekani.
"Huenda Afrika ikaathirika, ikiwa hatua hizi zitaathiri uchumi wa China au Marekani. Kama kuna shinikizo kwenye uchumi kutokana na hatua hii basi uchumi wa Afrika inaweza kuathirika kutokana na madhara ya mpito." Macharia alisisitiza
Macharia hata hivyo anasisitiza kuwa China iko kwenye nafasi bora kutokana na kuwepo kwa washirika wengi wa biashara, Afrika ikiwa mmoja wao. Aidha anashikilia msimamo kuwa Afrika inaweza kufaidika kutokana na mchakato huu.
Takwimu zinaonyesha kuwa China inaongoza katika soko ya utalii duniani kwani zaidi ya Wachina milioni 130 wanasafiri kote duniani kila mwaka ... idadi hiyo inaendelea kupanda. Na hii huenda ikawa faida kwa Afrika.
"Marekani inaweza kupoteza mengi iwapo China itawashauri wananchi wake dhidi ya kusafiri kwenda Marekani. Afrika na nchi nyingine zinazoendelea kwa upande mwingine zinaweza kufaidika kama China itawashauri wananchi wake kukumbatia utalii wa Afrika." Alisema
Katika jitihada zake za kusaidia kujenga jamii ya mafanikio ya pamoja, China imeshinikiza mifumo kama vile Mkanda mmoja Njia moja na BRICS. Juhudi hizi zimevutia mataifa mengi ya dunia ambayo hadi sasa zimetia saini kuwa wanachama. Ni rahisi kwa China kuwageukia kama washirika mbadala wa kibiashara iwapo malumbano kati ya Beijing na Washington yatashamiri.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |