Na Majaliwa Christopher
China itaendelea kuieleza dunia sababu, kiini na msingi wa mgogoro wa kibiashara kati yake na Marekani kupitia vyombo vyake vya habari.
Ikiwa ni miezi kadhaa baada ya kuanza kwa vita ya kibiashara kati ya mataifa haya mawili, China imesisistiza kuwa vyombo vyake vya habari vitaenda zaidi ya kuripoti mgogoro wenyewe, na badala yake, kuelezea chanzo na sababu za msingi za kuwepo kwa hali hiyo.
"Tutaendelea kutoa habari zisizokuwa na mrengo wowote wala kuegemea upande wowote. "
Ni muda muafaka kupitia kwa namna vyombo vyetu vinavyoandika na kutangaza hili suala dunia ikatambua ukweli wa chanzo cha mgogoro uko wapi," alisema Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari China, Bw. Rong Changhai.
Akizungumza na waandishi wa habari kutoka barani Afrika walio katika programu maalum ya mafunzo walipotembelea ofisi za chama hicho jijini Beijing, Bw. Rong alisema vyombo vya habari nchini China vina wajibu wa kuelezea dunia chanzo na sababu za kuwepo kwa mgogoro huo wa kibiashara.
Alisisitiza kwamba China kupitia kwa vyombo vyake vya habari, imekuwa mara kadhaa, ikisisitiza umuhimu wa kuondokana na huo mgogoro kwa kuelezea namna bora ya kuushughulikia.
Bw. Rong alisema kuwa wanaenda mbali zaidi katika kuandika na kutangaza habari za mgogoro huo tofauti na unavyofanywa na vyombo vya nchi zingine kwa kuelezea kwa kina ulivyoanza, unapoelekea na namna bora ya kuutatua huku dunia ikiachwa ichambue na kuona ukweli wake ulivyo.
"Sisi hatufundishi watu namna ya kuamua. Tunawapa sababu, chanzo na habari za kina zilizofanyiwa utafiti wa kutosha ili wao wenyewe waweze kuamua. Hii ndiyo kazi yetu ya msingi...tunaegemea katika misingi ya uandishi wa habari," aliendelea kusisitiza.
Alieleza kuwa msimamo wa serikali ya China juu ya vita ya kibiashara kati yake na Marekani iko wazi na hata juhudi zake za kuitafutia ufumbuzi tokea mwanzo uko wazi na ndicho ambacho vyombo vya habari vinatangaza na kuandika.
Ni miezi kadhaa sasa tangu China na Marekani ziingie katika mgogoro wa kibiashara huku dunia ikishuhudia pande zote mbili zikiwekeana vikwazo.
Mgogoro huu ulishika kasi zaidi hapo mwezi Machi ambapo Marekani ilitangaza kuweka kodi mpya kwa bidhaa kutoka China zenye thamani ya dola bilioni 60.
Siku chache baadae, China kwa upande wake pia ilitangaza hatua ya kukabiliana na hali hiyo, ikiweka bayana kuwa itatoza kodi bidhaa za Marekani 128, zenye thamani ya dola bilioni 3.
Pamoja na Shirika la Biashara Duniani (WTO) kuonya kuhusu athari ambazo zinaweza kuikumba dunia kutokana na hali hii bado inaoneka hakuna ufumbuzi wa karibu huku Marekani ikiendelea kuchukua hatua mbalimbali za 'makusudi' za kuendelea kuweka vikwazo kwa China.
China mara kadhaa imekuwa ikisisitiza kuwa iko tayari wakati wowote na kwa namna yoyote kupambana na hali yoyote itakayoonekana kugusa maslahi yake kivivyote vile.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |